Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali kuanzisha Tume ya Taifa ya Ardhi kumaliza migogoro

New Content Item (1)

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deo Ndejembi.

Muktasari:

  • Waziri Ndejembi akiri kuwa migogoro ya ardhi nchini bado ni tatizo sugu, hivyo Serikali imeona njia ya kumaliza hayo ni Tume ya Taifa ya Ardhi.

Dodoma. Serikali iko mbioni kuanzisha Tume ya Taifa ya Ardhi (Land Commission), ikieleza itakuwa mwarobaini wa kuondoa migogoro.

Kauli hiyo imetolewa leo, Ijumaa Mei 23, 2025, na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deo Ndejembi, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za wizara kwa kipindi cha miaka minne.

Waziri Ndejembi amekiri kuwa migogoro ya ardhi nchini bado ni tatizo sugu, hivyo Serikali imeona njia ya kumaliza tatizo hilo ni kuunda Tume ya Taifa ya Ardhi.

Amesema kumekuwa na mwingiliano wa taasisi nyingi kwa wakati mmoja, hasa kwa watu wanapotaka kujenga, ambapo mpimaji wa ardhi ni wizara, lakini anayetoa kibali cha ujenzi ni halmashauri, jambo ambalo linatoa mkanganyiko.

“Kwanza, tumechelewa sana. Tulipaswa kuwa na chombo hiki muda mrefu, ndiyo maana mambo yamekuwa kama yalivyo sasa, lakini hii itamaliza kabisa,” amesema Ndejembi.

Katika hatua nyingine, Waziri Ndejembi amesema uholela umezidi katika wizara kwa wanaojiita madalali, ambao wamesababisha migogoro katika maeneo mengi ambako watu wanauza viwanja kwa watu zaidi ya mmoja.

Waziri amesema hakuna chombo maalumu cha kuwasimamia madalali hao, ambao baadhi yao wanakuwa ni watumishi wa halmashauri, na kwamba mambo mengine yalibainika kwenye kliniki za ardhi.

Kwa mujibu wa waziri, yote hayo yanakwenda kuisha kama tume hiyo itaanza, kwani maeneo mengi yatapangwa kwa kuwashirikisha wananchi.

Amesema kwa sasa wizara inafanya mpango wa kupiga picha za anga ili kupata ramani mpya za kisasa, kwani maeneo mengi ambayo yanapangwa kwa sasa yanatumia ramani za mwaka 1970.

Kuhusu mahitaji ya nyumba, amesema wizara inaendelea kujenga nyumba katika maeneo mbalimbali nchini, kwani tathmini inaonyesha kuwa Tanzania inahitaji nyumba 380,000 kila mwaka, hivyo wataendelea kufanya shughuli zote kwa kushirikiana na sekta binafsi kumaliza kazi hiyo.