Serikali kuendelea kujenga maghala ya kuhifadhi mazao nchini
Arusha. Serikali imesema inaendelea kujenga maghala ya kuhifadhia mazao nchini ili kuzuia sumu kuvu hali inayochangia athari kwa wakulima na wazalishaji wa chakula.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli wakati akifungua kikao cha wadau wa sekta ya kilimo jijini Arusha kilichowakutanisha washiriki kutoka nchi 11, ambapo amesema ni lazima kuwepo kwa mifumo thabiti itakayosimamia masuala mazima ya kilimo na utoshelezi wa chakula.
Aidha Tanzania imepata dola za kimarekani 20 milioni zilitolewa kama msaada wa mapambano ya sumu kuvu licha ya kuonekana athari za awali ,kupitia fedha hizo tayari serikali imekwishajenga maghala na maabara katika baadhi ya maeneo ya mikoa ikiwemo Manyara, Morogoro na Dodoma ambayo wakulima wake walikumbana na tatizo hilo.
Mweli amesema walianza kujenga maghala hayo katika mikoa ya Manyara, Morogoro na Dodoma kutokana na tatizo hilo kuonekana kuwa kubwa katika mikoa hiyo ambapo walishajenga maghala 10 katika mikoa mbalimbali ya Tanzania na maabara mbili za kupima sumu kuvu.
Ameongeza baada ya mkutano huo washiriki watapaswa kukaa pamoja kuweka mikakati mizuri ya kufanya katika kusaidia wakulima namna bora ya kuhifadhi mazao na kuondokana na tatizo hilo la sumu kuvu katika nchi hizo.
"Tumekubaliana kuwa baada ya mkutano huu washiriki ambao miradi hii inatekelezwa katika nchi zao waweke mfumo mzuri wa kuwaelimisha wakulima na wazalishaji wa chakula juu ya uwepo wa sumu kuvu lakini pia ifike mahali tusiagize tena vyakula nje tuweze kuwa na uzalishaji unaotosheleza" amesema Mweli.
Naye Mwakilishi kutoka Benki ya Maendeleo Afrika, Philip Boahen amesema kutokana na uzalishaji wa chakula kushuka barani Afrika kutokana na kipindi cha COVID-19 waliamua kutoa mkopo huo ili kuinusuru hali ya chakula hivyo amesema lengo ni kuinua uzalishaji kwa kasi.
"Tunajua namna gani uzalishaji wa chakula ulishuka kutokana na janga la Corona hivyo tumeona ni vema kuliangalia suala la uzalishaji wa chakula na kuwekeza katika miradi hii ambapo tuna nchi 13 zinazotekeleza programu hii" amesema Boahen
Aidha mkutano huo ambao ni wa siku nne umezikutanisha nchi 11 ambazo zimeweza kutuma washiriki katika mkutano huo huku mkutano huo ukiratibiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika .