Serikali kufanya ukarabati mkubwa wa jengo la abiria JNIA

Muktasari:

  • Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imesema ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato kitakuwa kiwanja cha nne cha kimataifa huku wakitarajia kufanya ukarabati mkubwa wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Dodoma. Serikali itaanza ukarabati mkubwa katika jengo la abiria kwenye uwanja wa ndege wa pili wa ha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere (JNIA- terminal 2) ifikapo Juni mwaka 2023.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Mussa Mbura ameyasema hayo leo Jumapili Oktoba 30, 2022 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato jijini Dodoma.

Amesema mbali na JNIA viwanja vingine vinavyoendelea kukarabatiwa nchini ni pamoja na Arusha, Songwe, Ruvuma, Bukoba, Mwanza, Songea, Dodoma, Mtwara, Iringa, Tabora Kigoma, Mafia, Mpanda na Geita.

Amesema ukarabati huo utalifanya jengo hilo liwe la kisasa zaidi lakini pia litaunganisha kati ya Terminal Two na Terminal Three.

“Tuna mpango wa kulitumia jengo hilo kama hub (kituo) ya kampuni yetu ya ndege ya Tanzania (ATCL).

“Ukarabati huu ni mafanikio ya matunda ya ziara yako (Rais Samia Suluhu Hassan) ulioifanya nchini Ufaransa Februari 2022,” amesema.

Amesema ujenzi wa Kiwanja cha Kimataifa cha Msalato jijini Dodoma utakifanya kiwanja hicho kuwa kiwanja cha nne cha kimataifa Tanzania.

Aidha, Mbura amesema hadi kufikia Machi mwaka jana Tanzania ilikuwa na viwanja vya ndege 435 ambapo kati ya hivyo 194 vinamilikiwa na Serikali.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema jumla ya wakazi 3,368 wamelipwa Sh16.93 bilioni kupisha ujenzi wa kiwanja hicho.

Amesema wapo watu 10 ambao wanadai fidia ya Sh80 milioni ambayo malipo yao yameshapelekwa hazina kwa ajili ya malipo.