Serikali kufufua mashamba ya maua, mbogamboga na matunda Arusha

Mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongella (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Horticultural Association (Taha),Jacqueline Mkindi akikagua shamba la Kiliflora (Loliondo) eneo la Usa River wilayani Arumeru. Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Serikali mkoani hapa itashirikiana na wadau mbalimbali kutafuta ufumbuzi wa mashamba makubwa yaliyosimamisha uzalishaji wa mazao ya maua, mbogamboga na matunda ili kurejesha ajira zilizopotea na kuongeza mapato ya serikali.

Arusha. Mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongella amesema Serikali itashirikiana na wadau kutafuta ufumbuzi wa mashamba makubwa yaliyosimamisha uzalishaji wa  mazao ya maua, mbogamboga na matunda ili kurejesha ajira zilizopotea na kuongeza mapato ya Serikali.

Katika ziara iliyoratibiwa na Chama cha Wazalishaji wa Mbona na matunda (Taha) wilayani  Arumeru na jijini Arusha kukagua mashamba yanayoendelea na uzalishaji na yaliyositisha uzalishaji wake amesema mchango wa sekta ya kilimo cha maua, mbogamboga na matunda ni muhimu kufufuliwa kwa manufaa ya nchi.
Amesema maelekezo ya Serikali ni kuhakikisha sekta za kiuchumi zinatoa mchango mkubwa zaidi kwa serikali kuendelea kutimiza wajibu wake wa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji kufikia malengo yao na kushughulikia changamoto zinazokwaza uwekezaji.
“Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo tuhakikishe sekta za kiuchumi zinazozalisha zijengewe uwezo ili zizalishe zaidi ili kukuza mapato ya nchi na kuongeza ajira,changamoto ya mashamba haya kusimamisha uzalishaji tutangalia yale ambayo ngazi ya mkoa tunaweza kufanya,” amesema Mongella.
Mongella alisema maua,mbogamboga na matunda ni mazao yenye thamani ya juu kwenye soko la dunia hivyo ufufuaji wa mashamba hayo utachangia mapato katika uchumi wa nchi kutokana  na kuwa na mnyororo mkubwa wa thamani kwenye uchumi.
Mkurugenzi Mkuu wa Taha,Jacqueline Mkindi  amesema  sekta ya kilimo wilayani Arumeru awali ilikua ikichangia mapato mengi lakini baada mashamba hayo kuacha uzalishaji mapato yaliyokua yanapatikana yalishuka kwa kiwango kikubwa.
Amesema sekta hiyo ikisimamiwa vizuri na kushughulikia changamoto zinazorudisha nyumba mazao ya maua, mbogamboga na matunda inaweza kuingiza zaidi ya dola 3 bilioni kwa mwaka ukilinganisha na dola 700 milioni zinazopatikana kwa sasa.