Serikali kufungua kampasi ya UDSM mkoani Lindi

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda
Muktasari:
Katika kuhakikisha inasogeza huduma ya elimu kwa wananchi hivi karibuni Serikali inatarajia kufungua kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mkoani Lindi.
Dar es Salaam. Katika kuhakikisha inasogeza huduma ya elimu kwa wananchi hivi karibuni Serikali inatarajia kufungua kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mkoani Lindi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda ameyasema hayo leo Jumatano Februari 09, 2022 wakati akielezea mafanikio ya wizara hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu madarakani.
“Haya ni maelekezo ya Rais Samia kuwa tuhakikishe elimu ya juu inasogezwa hasa katika mikoa ambayo haina vyuo vikuu. Nitaenda Lindi kutembelea kuona ulipofikia mradi huu,” amesema bila kubainisha kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya ujenzi huo.
Amebainisha kuwa Serikali katika kipindi cha mwaka mmoja imeongeza bajeti ya mkopo wa Elimu ya juu kutoka Sh464 bilioni kufika Sh570 bilioni na kuondoa asilimia 6 ya ongezeko la thamani na kufuta asilimia 10 ya ongezeko mtu anapochelewa kulipa mkopo.
Profesa Mkenda amesema Wizara imepatiwa Dola za Kimarekani milioni 425 sawa na Sh970 bilioni ili kuboresha vyuo vikuu vya umma na Taaisis za elimu ya juu hapa nchini.
Amesema wamepewa Sh8.9 bilioni kuimarisha elimu ya juu katika sayansi husuani katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).
Akizungumzia mafanikio upande wa mafunzo na ufundi stadi, amesema Serikali inajenga chuo kikubwa cha Ufundi jijini Dodoma chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3000.
"Tunajenga chuo kikubwa sana cha ufundi pale Dodoma, ambacho kitachukua wanafunzi 3,000, tunazo Sh17.9 bilioni, hizi ni jitihada za Serikali inayoongozwa na Rais Samia kuona umuhimu wa kuwapa wanafunzi uwezo wa kujiajiri,” amesema.
Aidha amesema vyuo vya Veta 25 vitajengwa katika wilaya mbali mbali nchini lakini pia kujenga vingine vipya katika mikoa minne ya Geita, Simiyu, Njombe na Ruvuma.
“Hatua hii ni kutekeleza agizo la Rais Samia la kujenga Veta katika mikoa ambayo haina vyuo hivyo,” amesema akiongeza kuwa pia vyuo vya ufundi vingine 12 vinafanyiwa ukarabati.