Serikali kuiburuza JATU kwa vyombo vya Dola

Serikali kuiburuza JATU kwa vyombo vya Dola

Muktasari:

  • Hatua hiyo imekuja kufuatia kikao cha Waziri Bashe na baadhi ya wanachama wa JATU PLC kilichofanyika jijini Dodoma, Aprili mwaka huu.

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema wizara yake imekamilisha uchunguzi kwa kampuni ya Jenga Afya Tokomeza Umasikini (JATU) PLC na kwamba ripoti ya uchunguzi hiyo itakabidhiwa kwa vyombo vya Dola wiki hii.

 Kauli ya Waziri Bashe imekuja kufuatia malalamiko ya wanachama wa kampuni hiyo, wakihofu kutapeliwa mabilioni ya fedha waliyowekeza kwenye kampuni hiyo inadai kuwalimia mazao na kuwafugia mifugo.
Akiandika katika ukurasa wake wa Twitter leo Agosti 16, Waziri Bashe amesema;
“Naomba niwataarifu wakulima waloleta Malalmiko yao kuhusu JATU PLC kuwa team ya Wizara imekamilisha kazi yake, Report itakabidhiwa kwenye vyombo vya Dola wiki hii kwa hatua zaidi. NB: Nasisitiza wanaotaka kuwekeza kwenye kilimo Jiridhishe kwanza.”
Amewawatahadharisha Watanzania wanaoshawishika kuwekeza kwenye kilimo kupitia mitandao ya jamii, akiwataka kujirisha kwanza.
Ameendelea, “Pesa zako unakabidhi kwenye taasisi gani, Je hayo maeneo wanayokuambia watakulimia umeyaona? Umeyatembelea? Je Halmashauri husika ama Wizara ya kilimo inatambua hicho kitu? Kumekua na watu wengi wakija wizarani baada ya kupata athari ya kupoteza pesa zao.”
Waziri Bashe amesisitiza hakuna kilimo cha Whatsup or Instagram or twitter.
“Kama una fedha zako nenda kajiridhishe hicho ulichakiona mtandaoni, nunua ardhi yako ajiri mtu/watu usikubali hizi habari leta 10 milioni nikakulimie utapata 15 milioni. Nasisitiza hakuna kilimo cha whatsup. Nenda shambani mwenyewe.”
Amewataka wakulima kuwasiliana na ofisi za wizara ya kilimo katika Idara ya Maendeleo ya Biashara Masoko na Huduma kwa wateja ili kupaya msaada.