Serikali kuongeza kasi kuwafikia wanaotaka kujifunza Kiswahili duniani

Dar es Salaam. Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema ameamua kutembelea Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) ili wajadaliane na kuongeza kasi ili kuwafikia watu wengi zaidi.

Msigwa ameyasema hayo leo Oktoba 12,2023, katika ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

Amesema lugha ya Kiswahili ina wazungumzaji takribani milioni 500 duniani kote ipo haja ya kuweka utaratibu mzuri zaidi kuwafikia ili wazungumze lugha sanifu na fasaha.

"Kuna wazungumzaji milioni 500 kutoka mataifa mbalimbali na juhudi zaidi tumeweka kufundisha katika ofisi za ubalozi, lakini wapo watu wengi wanafundisha wasio na taaluma, sisi serikali tunataka kuwafikia watu wote wanaopenda kujifunza ili wajifunze Kiswahili sanifu," amesema.

Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi amesema baraza hilo limekuwa katika mikakati mbalimbali ili kuhakikisha makundi mbalimbali wanafikiwa na huduma za Kiswahili.

Amesema tangu Kiswahili itangazwe siku ya Kiswahili Duniani, fursa za Kiswahili zimeongezeka, huku mataifa mengi ya Afrika na nje ya bara hili yakipanua wigo zaidi kuhitaji huduma hiyo.

"Baraza limekuwa lihakikisha linaendelea kusimamia, kuratibu na kuendeleza Kiswahili kitaifa, kikanda na kimataifa," amesema.