Serikali kurejesha mafuvu ya viongozi wa kimila kutoka nje

Saturday January 22 2022
mafuvupic
By Janeth Joseph
By Florah Temba

Moshi. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Maliasili na Utalii wanaendelea na majadiliano ya urejeshwaji wa mafuvu ya viongozi wa kimila yaliyochukuliwa na wakoloni.

Rais Samia ameitoa kauli hiyo leo Jumamosi Januari 22, 2022 baada ya Mwenyekiti wa machifu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Frank Marialle kumwomba urejeshwaji wa mafuvu hayo ili yatumike kuendeleza historia na utalii katika mkoa huo.

"Mmeomba kuyarejesha nchini mafuvu ya machifu yaliyochukuliwa wakati wa ukoloni ili yatumike kuelimisha jamii na shughuli za kitalii, Sserikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya maliasili na utalii wanaendela na majadiliano ya urejeshwaji wa mafuvu hayo tutakapofanikiwa tutawaarifu," amesema Rais Samia.

Akisoma risala ya umoja wa Machifu Mkoani hapa, Frank Marialle ameiomba Serikali kuzisaidia familia ambazo mafuvu ya viongozi wao wa kimila yaliyochkuliwa na wakoloni yarejeshwe.

"Tunaiomba serikali kusaidiana na machifu wa Kilimanjaro na Tanzania kwa ujumla kuzisaidia familia ambazo mafuvu ya viongozi wao wa kimila wa wakati huo yaliyochukuliwa na wakoloni hasa wajerumani ili yaweze kurejeshwa na yatumike kuendeleza Historia na utalii katika Mkoa na kuongeza kipato kwa  jamii na serikali kwa ujumla," ameeleza Marialle.

Advertisement
Advertisement