Serikali kushusha bei ya gesi

Muktasari:

  • Kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya siku ya haki za mtumiaji zimefanyika leo jijini Mbeya ikiwa na kaulimbiu ya ‘Nishati safi kwa ustawi wa mtumiaji na mazingira’.

Mbeya. Serikali imesema iwapo mipango ya kuongeza uzalishaji umeme itakwenda kama inavyokusudiwa itasaidia kupunguza gharama za matumizi ya gesi kwa wananchi wa kipato cha kati na chini.

Hayo yameelezwa leo Machi 15 na Naibu Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Exaud Kigahe kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo, Dk Ashatu Kijaji wakati wa kongamano la maadhimisho ya kitaifa ya siku ya haki za mtumiaji duniani yaliyofanyika jijini hapa.

Kigahe amesema Serikali kama chombo chenye wajibu wa kutekeleza miradi ya nishati safi ya gesi ni kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa wananchi wote na kwa gharama nafuu ili kukuza kipato.

Amesema iwapo Serikali itafanikiwa kuzalisha na kutumia kwa wingi nishati safi gaharama za uzalishaji zitapungua na kuwa na viwanda shindani kikanda na kimataifa na kwamba hiyo ndio dira ya Taifa.

Ameleeza kuwa mkakati mkubwa wa kitaifa ni kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya uzalishaji wa umeme wa megawati 10,000 kwa njia ya gesi asilia ifikapo 2025.

“Hivyo natoa rai kwa Tume ya Ushindani (FCC) kushirikiana kwa karibu na sekta za uzalishaji wa nishati kama Baraza la Usimamizi na Utunzaji Mazingira (NEMC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kuhusiana na matumizi ya nishati safi, zisizoharibu mazingira wala kuathiri ustawi kwa mtumiaji,” amesema Kigahe.

Kigahe amewataka watoa huduma wanaotumia mikataba ya kutoa huduma ya nishati jadidifu kuwasiliana na tume ya ushindani kuhakikisha wanatambulika kwa kusajiliwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), William Erio, Zaytun Kikula amesema ulimwengu wa sasa unatawaliwa na jamii inayotumia nishati kwa ustawi wao katika maeneo mbalimbali akitaja changamoto zinazowakabili watumiaji.

“Nishati inapatikana kwa gharama kubwa ambayo wengi hawawezi kuimudu, Taasisi ya Kulinda Watumiaji Duniani (Consumers International) imebainisha kuwa bei ya nishati ilipanda kwa asilimia 50 kufikia mwishoni mwa mwaka 2022 na itaendelea kupatikana kwa gharama kubwa katika mwaka wote wa 2023,” amesema.

“Kupanda kwa gharama za nishati, hupandisha gharama za maisha na kuwasukuma watumiaji kutumia nishati zinazoharibu mazingira kama vile kuni na mkaa, hasa katika nchi zinazoendelea na kukosa uelewa,” amesema Zaytun.

Amefafanua kuwa kutokana na changamoto hizo, FCC katika kuadhimisha kilele cha maadhimisho mwaka huu imefanya shughuli mbalimbali zauelimishaji umma juu ya matumizi ya nishati safi.

Nao baadhi ya washiriki wa kongamano hilo wameshauri kuwapo kwa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi juu ya matumizi ya gesi safi huku wakiomba serikali kuangalia gharama za gesi.

“Tumesikia serikali kuja na mpango wa matumizi ya mabomba ya gesi hadi sasa wananchi wa chini hawajui itakuaje ukilinganisha na ile ya kuweka kwenye mitungi, nashauri elimu itolewe lakini waangalie na gharama zake kwa wananchi,” amesema Trifonia Kabende.