Serikali kutoruhusu uhaba wa sukari 2021

Serikali kutoruhusu uhaba wa sukari 2021

Muktasari:

  • Wakati baadhi ya wazalishaji wa sukari wakidai ucheleweshaji wa vibali vya kuagiza kuwa ndiyo sababu ya kutokea uhaba wa sukari, Serikali imesisitiza mwaka huu hawaturuhusu tatizo hilo litokee.

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wazalishaji wa sukari wakidai ucheleweshaji wa vibali vya kuagiza kuwa ndiyo sababu ya kutokea uhaba wa sukari, Serikali imesisitiza mwaka huu hawaturuhusu tatizo hilo litokee.

Kila mwaka viwanda vya sukari nchini husimamisha uzalishaji katika mwezi wa Machi kutokana na kuwapo kwa mvua ambazo huathiri kiwango cha uzalishaji wa miwa na hatimaye kusababisha uhaba wa sukari nchini

Ni wakati huo, ambao viwanda hutumia fursa hiyo kufanya ukarabati.

Hata hivyo, Serikali imesema inaweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa mwaka huu uhaba wa sukari hautokei.

Tayari kumekuwapo na mazungumzo huku, Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe akikutana na wadau wa sukari Januari 29 jijini Dodoma

Lakini jana akizungumza kwa simu na Mwananchi, Mwenyekiti wa bodi ya kiwanda cha sukari cha Kilombero kilichopo mkoani Morogoro, Ami Mpungwe alisema licha ya mikakati ya kiwanda hicho kuongeza uzalishaji, wana changamoto cha kucheleweshewa vibali vya kuagiza sukari na Serikali.

“Ukweli ni kwamba uzalishaji wa viwanda vya ndani bado ni mdogo na kila mwaka mahitaji ya sukari yanaongezeka kwa sababu watu wanaongezeka.

“Tatizo kubwa kuanzia Machi hadi Aprili masika yanaanza, kwa hiyo ni lazima tupate vibali vya kuagiza in good time (wakati mzuri). Tatizo hatupati vibali kwa wakati,” alisema Mpungwe.

Aliendelea; “Kwa mfano mwaka juzi tuliomba vibali Novemba, tumekuja kupewa Machi. Safari hii tumeomba vibali Desemba, lakini mpaka sasa hatujapewa,” alisema.


Ufafanuzi wa Serikali

Juhudi za kumpata Waziri Mwambe kufafanua undani wa mazungumzo yake na wazalishaji hao hazikufanikiwa kwani kila alipopigiwa simu, hakupokea wala kujibu ujumbe.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ambaye pia wizara yake inahusika na sekta ya sukari alizungumza na Mwananchi jana na kukiri kuwa wizara hiyo imepokea maombi ya vibali kuagiza sukari nje ya nchi na kusema kuwa bado vinashughulikiwa.

“Sisi kama wizara tuko kwenye mchakato wa kuvishughulikia. Pili, kwa kuwa mahitaji yanajulikana, Wizara kupitia Bodi ya Sukari Tanzania tutaweka utaratibu wa kuhakikisha sukari inapatikana mapema. Kwa hiyo, mwaka huu hatutegemei kuwa na upungufu wa sukari,” alisema.

Alipoulizwa sababu ya kuchelewa kwa vibali hivyo, Waziri Bashe alisema kuna wizara hiyo imekuwa ikifanya tathmini ya uzalishaji wa sukari na uagizaji ili kuhakikisha wakulima wadogo wanafaidika.

Katika kipindi cha takribani miaka mitano hasa kila ikifika Machi hadi Juni, ambapo viwanda hufungwa, kumekuwa kukitoka tatizo la uhaba wa sukari.Hatua hiyo imekuwa ikisababisha bei ya sukari kupanda. Kwa mfano, mwaka 2016 bei ilipanda kutoka Sh1,800 kwa kilo hadi 3,000.