Serikali kuviunganisha vyo 35 vya ualimu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa Tehama wa 'School Connectivity' kwa shule 10 za sekondari za Serikali kwenye mikoa 10 uliondaliwa na Shirika la African Child Project kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania Foundation. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema itaviunganisha vyuo vyote 35 vya ualimu nchini katika mkongo wa Taifa ili kuendana na mabadiliko ya Kiteknolojia.
Moshi. Serikali imesema itaviunganisha vyuo vyote 35 vya ualimu nchini katika mkongo wa Taifa ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.
Mpaka sasa Serikali imeshaviunganisha vyuo vinne vya ualimu na mkongo huo wa Taifa ambapo mwaka 2021/22 vyuo vingine 15 vitaunganishwa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati wa uzinduzi wa mradi wa Tehama wa ‘School Connectivity’ kwa shule 50 za sekondari za Serikali kwenye mikoa 10 uliondaliwa na Shirika la African Child Project kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania Foundation.
"Pamoja na kuviunganisha vyuo hivi 35 kwenye mkongo wa Taifa tayari tumesambaza komputa 1,233 kwenye vyuo vyote vya ualimu vya Serikali ili kuwawezesha walimu tarajali kupata ujuzi unaotakiwa kuhusu Tehama,"
Profesa Mkenda amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mwalimu anayemaliza vyuo vya ualimu nchini anakuwa na ujuzi wa Tehama na kuitumia kufundishia wanafunzi wa shule za sekondari na msingi.
Amesema serikali kupitia mradi wake wa kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari itawezesha ufundishaji na ujifunzaji kidigitali katika maeneo mbalimbali ikiwa ni kuandaa mkakati wa Tehama wa elimu ya sekondari.
"Mkakati huu utanufaisha makundi yote ikiwa ni pamoja na walimu na wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule 1,500 za sekondari,"amesema Profesa Mkenda
Pamoja na mambo mengine, Waziri Mkenda amesema mradi huo utawezesha mafunzo kuhusu moduli za Tehama kwa walimu 4,000 kutoka shule za sekondari 2,000 nchini.
"Serikali inaendelea kuweka msisitizo maeneo mbalimbali ya sayansi na teknolojia ili kuwawezesha Watanzania kuendana na mabadiliko ya teknolojia, miongoni mwa majukumu hayo ni kuandaa mitaala ya elimu, miongozo, kutunga sera zinozohusu matumizi ya Tehama na teknolojia saidizi," amesema Profesa Mkenda
"Wizara inaendelea kuwajengea uwezo walimu wa sekondari na msingi pamoja na wakufunzi wa vyuo vya ualimu kuhusu matumizi ya Tehama kama nyenzo ya kujifundishia na kujifunzia,"
"Hadi kufikia 2021 zaidi ya walimu 1,693 ambapo kati ya hao wakufunzi na walimu wa shule za sekondari na msingi wenye mahitaji maalumu ni 350, wakufunzi wa vyuo vya ualimu wapatao 1,698 tayari wamepata mafunzo kazini na Tehama kwa lengo la kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa walimu tarajali,"
Naye ,Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha mradi wa African Child, Catherine Kimambo amesema mradi huo utawafikia wanafunzi 43,291 kwenye shule 50 na kutoa mafunzo kwa walimu 100 wa Tehama ambapo lengo ni kusaidia kuongeza ufaulu kwa asilimia 5 kwa mwaka.
"Tutatoa komputa 186 tablets 246, ruta 50 kwa ajili ya kuunganisha inteneti za simu zenye Gb 50 kila mwezi ndani ya mwaka mmoja kutoka Vodacom Tanzania Foundation na ujuzi wa kidigitali ambao utatolewa na wanafunzi kutoka DIT," amesema Kimambo
Amesema mikoa ambayo itanufaika na mradi huo ni Kilimanjaro, Kigoma, Katavi, Tabora, Morogoro, Tanga, Mara, Ruvuma, Njombe na Iringa.
Mkurugenzi wa Uhusiano Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia amesema katika kuhamasisha ufaulu wa wanafunzi katika shule za Serikali kwa matumizi ya Tehama wanatarajia kuwafikia wanafunzi zaidi ya milioni moja katika shule 1,500.
"Hadi sasa tumefikia shule 450 na kupitia mradi wa Vodacom Tanzania Foundation, hadi sasa tuna mwelekeo mpana zaidi ambapo tunataka kuzifikia shule 1500 Tanzania nzima na tutawafikia wanafunzi zaidi ya milioni moja kwa upande huu wa elimu," amesema