Serikali kuwachukulia hatua askari, yalipa fidia waathirika
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohammed Mchengerwa akikabidhi sehemu ya fedha kama pole kwa wananchi wa Kijiji cha Mwanavala waliojeruhiwa kwa kupigwa na Askari wa Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa) ambapo jumla alitoa Shilingi milioni tano. Picha na Hawa Mathias.
Muktasari:
- Hekta 34,000 kumegwa eneo la hifadhi kukabidhiwa wananchi Mbarali.
- Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohammed Mchengerwa ametoa kauli hiyo jana Mei 12, 2023 katika Kijiji cha Mwanavala Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya, huku akimuagiza Katibu Mkuu Wizara hiyo kuwachukulia hatua askari waliohusika washambulia kwa kipigo wananchi watano wakiwepo wanawake watatu.
Mbeya. Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohammed Mchengerwa amesema Serikali inatarajia kuweka GN 28 mpya katika eneo lenye ukubwa wa hekta 34,000 ambalo imeridhia kurejeshwa kwa wananchi wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
Mchengerwa amesema jana Mei 12, 2023 alipofanya ziara Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya baada ya kuzungumza na wananchi sambamba na kutoa pole kwa waathirka watano wakiwepo wanawake wawili waliojeruhiwa kwa kipigo na Askari wa Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa) Mei 7 mwaka huu sambamba na kutoa Sh5 milioni.
“Nimemuagiza Katibu Mkuu wizarani kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wote waliohusika na tukio hilo kwani Rais Samia Suluhu Hassan hapendi kuona wananchi wakiishi pasipo furaha na hatupendi matukio hayo kujitokeza Tanzania,”amesema.
Ameongeza kuwa “Hatujazoea kuona wala kusikia matukio ya aina hii kwa nchi ya Tanzania na hatuko tayari kuvumilia matukio ya ovyo ovyo yakitokea miongoni mwa jamii, nawataka wananchi pindi yakiendelea kutokea toeni taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Wilaya na Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM,”amesema.
Katika hatua nyingine, Mchengerwa amesema Mei 15 mwaka huu siku ya Jumatatu wataweka GN 28 mpya katika eneo lililomegwa kwenye hifadhi na kurejesha kwa wananchi sambamba na kutangaza rasmi, licha ya wananchi kuingia ndani ya hifadhi umbali wa kilometa 10.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema Serikali tayari inaendelea kutenga maeneo ya viwanja kwa ajili ya makazi ikiwepo maeneo salama ya mifugo.
“Bado tunaendelena kufuatilia mashamba ya Lanchi ya Usangu kubaini uhalali kufuatia baadhi ya watu kujimilikisha maeneo makubwa ya zaidi ya hekari 3,000 kwa kilimo na ufugaji,” amesema.
Mfugaji wa Kijiji cha Mwanavala, Lengai Samweli ameiomba Serikali kuwatengea eneo kwani wamekuwa wakichukiwa na kufanyiwa vitendo vya kikatili na kufukuzwa mara kwa mara jambo linalosababisha kuichukia na kujiona kama siyo raia wa Tanzania.
“Wakati tunaingia katika Kata hii kuna vitongoji vitano ambavyo tunaishi jamii ya wafugaji sasa Serikali ilikuwa wapi miaka yote kuwaondoa jambo ambalo inaonyesha wazi kuwachukia wafugaji,”amesema.
Awali Mei 11, 2023 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliagiza watendaji wa ngazi za Juu katika Wizara ya Maliasili na Utalii na Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa) na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera, kwenda Wilaya ya Mbarali kushughulikia mgogoro wa wananchi na hifadhi uliopelekea watu watano kujeruhi wakiwepo wanawake watatu.
Majaliwa alifikia hatua hiyo, baada ya Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Francis Mtega kuomba kikao cha Bunge mjini Dodoma kuhairishwa na kujadili tukio la wananchi kushambuliwa kwa kipigo hususan wanawake kuvuliwa nguo na kuchomwa na mapanga ya moto.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Christian Musyani amesema bado wanawashikilia askari watatu wa Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa) kuhusika na tukio hilo.