Serikali kuwawezesha wanafunzi waliokumbwa na mafuriko

Muktasari:


  • Wizara ya Elimu na Tamisemi zimekubaliana kuwasaidia wanafunzi waliokwama kwa sababu ya mafuriko.

Dodoma. Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini na kusababisha mafuriko, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolijia na Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamismi) zimekubaliana jinsi ya kuwasaidia wanafunzi waliokwama kuendelea na masomo.

Mawaziri, Profesa Adolf Mkenda wa Elimu na Mohamed Mchengerwa wa Tamisemi wamekutana jana Jumatatu, Aprili 15, 2024 jijini Dodoma pamoja na manaibu wao na watendaji wengine wa wizara hizo kujadiliana, ili kupata ufumbuzi.

Waziri Mchengerwa amesema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, kuna baadhi ya wanafunzi wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na changamoto ya mafuriko.

“Kutokana na hali ya mafuriko yanayoendelea nchini, mimi na mwenzangu wa Wizara ya Elimu (Profesa Mkenda) tumekubaliana sasa tuna kazi ya kuja na mpango wa muda mfupi na muda mrefu wa kusaidia wanafunzi.

"Mpango huo utawawezesha vijana wetu wanaosoma shule mbalimbali ambao leo hii wamekwama kuendelea na masomo kwa sababu ya majanga ya mafuriko yanayoendelea kote nchini, hususani katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Katavi na mikoa ya kaskazini na kusini.”

Amesema katika kutekeleza hilo, wizara zimewaelekeza wataalamu kutoka wizara hizo kwenda nchi nzima kufanya tathimini na kujiridhisha kutokana na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya shule uliotokana na mafuriko hayo.

“Tutakuwa na mpango wa muda mfupi wa kuwawezesha watoto wetu wanaosoma katika shule ambazo zimeathirika, zimebomoka au kuchukuliwa ni na maji, mpango wa muda mfupi ni kuhakikisha tunawawezesha vijana hawa wasirudi nyuma katika kusoma na kuwatengenezea mazingira yatakayowafanya waendelee na masomo.

Naye Profesa Mkenda amesema Serikali itahakikisha inaweka mazingira ya wanafunzi wote ambao shule zao zimeathirika na mafuriko nchini kuendelea na masomo.

"Tumekutana kwa ajili ya utekelezaji sera, lakini kubwa lililo mbele yetu kwa sasa ni kuhakikisha tunawezesha wanafunzi waliokwama kuendelea na masomo kutokana na athari za mafuriko nchini  wanawezeshwa kuendelea na hii ni kwa shule zote na Serikali na binafsi," amesema Profesa Mkenda.