Serikali: watakaopandisha bei za vyakula mwezi mtukufu wa Ramadhani kukiona

Serikali: watakaopandisha bei za vyakula mwezi mtukufu wa Ramadhani kukiona

Muktasari:

  • Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, imewawashia taa nyekundu wafanyabiashara  watakaopandisha bei za vyakula wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani unaotarajiwa kuanza hivi karibuni, kila inapofika mwezi huo baadhi ya wafanyabishara hupandisha bei kwa ajili ya kujinufaisha wenyewe.

Unguja. Wakati mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ukitarajiwa kuanza hivi karibuni, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewaonya wafanyabiashara watakaopandisha bei za vyakula hususani vinavyotumika kwenye mfungo huo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Unguja leo Jumapili Aprili 11, 2021, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban amesema watakaopandisha bei hizo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Mimi binafsi nitazunguka katika maeneo mbalimbali ya biashara kujiridhisha kama kweli wafanyabishara wanafuata maeekezo ya serikali na ijulikane kwamba zipo adhabu kali watakaokiuka taratibu,” amesema waziri

Ili kuhakikisha bei hazipandi, waziri Shaaban amesema wameunda kikosi kazi kinachoshirikisha Tume ya Ushindani kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo na kuchukua hatua zinazostahili.

Licha ya Sheria ya Ushindani na Kumlinda Mlaji namba tano ya mwaka 2018 kutobainisha adhabu kamili anazotakiwa kuchukuliwa anayekwenda kinyume, waziri amesema faini hiyo watakayotozwa inaweza isiwe chini ya Sh milioni moja.

“Kumekuwapo na tabia ya muda mrefu ya baadhi ya wafanyabiashara wenye tamaa kutumia fursa ya mwezi mtukufu kupandisha bei kiholela hasa kwa bidhaa muhimu kama mchele, sukari na ngano.

“Tabia kama hizi kutaka kuchuma faida kupitia mgongo wa wanaofunga hazikubaliki na mara nyingi husababisha wananchi wenye wa maisha duni kutekeleza ibada yao ya funga katika mazingira magumu,” amesema

Kuhusu kupunguza kodi za bidhaa kama ambavyo huwa inafanyika kila mwezi mtukufu, Shaabani alisema safari hii hawajaondoa kodi kwa sababu inaonekana hata serikali inapoondoa kodi hizo lakini wafanyabiashara huwa hawashushi bei.

Naye Mfanyabiashara maarufu visiwani humo Mohamed Raza alisema wanaopandisha bei za vyakula hawana huruma na wananchi akidai bei za vyakula na kodi bado havijapanda.

 “Lazima tuwarahisishie wananchi kujikimu, waweze kula futari sio sisi (wafanyabiashara) kutumia fursa hii kuwakomoa, ushuru bao upo vilevile bei sokoni inakubalika ipo vilevile, tuwasaidiewananchi wapo wanaokula mlo mmoja kwa sababu hawana uwezo,” amesema