Serikali ya Kenya yapuuza madai ya Ruto

Mgombea urais wa United Democratic Alliance (UDA), William Ruto

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Fred Matiang’i amekanusha na kupuuza tuhuma za Naibu Rais William Ruto na mgombea urais wa Kenya Kwanza kwamba sekta ya usalama inatumiwa kuvuruga uchaguzi.

Kenya. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Fred Matiang’i amekanusha na kupuuza tuhuma za Naibu Rais William Ruto na mgombea urais wa Kenya Kwanza kwamba sekta ya usalama inatumiwa kuvuruga uchaguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari, leo Ijumaa, Agosti 5, jijini Nairobi huku akiwa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), George Kinoti, Matiang’i amesema tuhuma hizo hazina ukweli wowote ndiyo maana hazina ushahidi ambao mhusika ameutoa.
Waziri huyo amesema hakuna agizo lililotolewa kwa watumishi wa Serikali kusaidia kampeni za mgombea wa Azimio la Umoja, Raila Odinga hivyo tuhuma za Ruto ni za kisiasa.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii tunajikuta tukiitumikia serikali moja lakini tunajibizana kwenye vyombo vya habari, tunapaswa kuwa na adabu na heshima ya kutosha kwa ofisi tunazosimamia ambazo tumepewa na watu wa Kenya” amesema
‘Kwa miaka minne iliyopita tumeishi katika mazingira magumu ambapo mjumbe wa baraza la mawaziri mara kwa mara anashambulia sekta ya usalama ilhali anakaa katika baraza la usalama la taifa” amesema
Jana Ruto alifanya mkutano na waandishi wa habari na kumtuhumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kupanga mipango ya kuiba kura, kuwalazimisha wafanyakazi wa Serikali wamuunge mkono Odinga, kusambaza vipeperushi vya kumkashifu na kuwatisha baadhi ya watu walio kwenye timu yake ya kampeni.
Kenya inatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu, Agosti 9, 2022 na joto linazidi kupanda kila kukicha.