Serikali ya Tanzania kujenga shule 246 kwa siku 30

Muktasari:

  • Serikali inatarajia kujenga shule za sekondari 246 ndani ya mwezi mmoja kwa ajili ya kujiandaa na udahili wa wanafunzi waliomaliza darasa la saba.



Dodoma. Serikali inatarajia kujenga shule za sekondari 246 ndani ya mwezi mmoja kwa ajili ya kujiandaa na udahili wa wanafunzi waliomaliza darasa la saba.

Taarifa hiyo  imetolewa na katibu mkuu wa ofisi ya rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Profesa Riziki Shemdoe leo Jumanne Septemba 14, 2021 wakati akifungua mkutano wa tatu wa wakuu wa shule za msingi Tanzania Bara.

Profesa  Shemdoe amesema kufuatia Serikali kudahili wanafunzi wengi kutokana na utaratibu wa  elimu bila malipo,   wengi wametakiwa  kujiunga na kidato cha kwanza na sasa idadi imekuwa kubwa.

Amesema shule hizo zinatarajiwa kujengwa kwenye kila halmashauri,  "kabla ya mwisho wa mwezi huu tunakwenda kujenga shule za sekondari 246, mngeuliza kwanini sio shule za msingi, shule za msingi mtakumbuka kama mmedahili watoto wengi sana tulivyoanza elimu bila ada."

"Wanafunzi hao tunategemea kuwapokea  ni vyema tumeona tukaanza na shule za sekondari kwa ajili ya kuwapokea."