Serikali ya Tanzania yazungumzia msamaha wa kodi kwa taasisi za dini

Serikali ya Tanzania yazungumzia msamaha wa kodi kwa taasisi za dini

Muktasari:

  • Serikali imesema bado inaendelea kutathmini maombi ya kusamehe kodi kutoka kwa taasisi za dini ili kubaini hatua zinazoweza kuchukuliwa bila kuathiri matakwa ya sheria zilizopo.

Dodoma. Serikali imesema bado inaendelea kutathmini maombi ya kusamehe kodi kutoka kwa taasisi za dini ili kubaini hatua zinazoweza kuchukuliwa bila kuathiri matakwa ya sheria zilizopo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ameliambia Bunge leo Jumanne Mei 25, 2021 na kubainisha kuwa taasisi za dini zinazojiendesha kwa sadaka na misaada hazitakiwi kulipa kodi licha ya kusajiliwa na kuwa na namba ya mlipakodi.

Alikuwa akijibu swali la msingi la mbunge wa Vunjo (CCM),  Dk Charles Kimei aliyetaka kujua  kama Serikali haioni umuhimu wa kuzisamehe kodi za miaka ya nyuma taasisi hizo.

Kimei amesema taasisi zilizokuwa zikiendeshwa kwa utaratibu usiolenga kupata faida, ziliiwekewa utaratibu wa kuanza kulipa kodi.

Amesema  kwa mujibu wa sheria za kodi, taasisi za dini ambazo zinajiendesha kutokana na sadaka toka kwa waumini ama misaada ya ndani na nje ya nchi hazitakiwi kulipa kodi ya mapato kisheria.

Ametaja lengo la kujiandikisha na kupata namba ya mlipakodi huwa na madhumuni ya kuziwezesha kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu Mamlaka ya Mapato (TRA)kama vile kuwasilisha kodi zilizokatwa kutoka kwa watumishi kutoka kwa taasisi  hizo na usajili wa mali mbalimbali.

Dk Mwigulu amesema taasisi za dini zinazofanya shughuli za kiuchumi kwa lengo la kujipatia faida kutokana na shughuli hizo, zinatakiwa kusajiliwa TRA  kama wafanyabiashara wengine na kulipa kodi ya mapato kulingana na faida inayopatikana.