Serikali yaagiza halmashauri kujenga vyumba vya kujisitiri wanafunzi

Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), David Silinde akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu, bungeni jijini Dodoma, Novemba 8, 2022.

Muktasari:

Katika kukabiliana na changamoto ya watoto wa kike kukosa masomo, Serikali imeziagiza halmashauri zote kujenga vyumba vya kujisitiri kwa wanafunzi wa kike ili kuwasaidia wakati wakiwa katika hedhi na hivyo kutokosa masomo.

Dodoma. Serikali imeziagiza halmashauri zote kujenga vyumba vya kujisitiri kwa wanafunzi wa kike ili kuwasaidia wakati wakiwa katika hedhi na hivyo kutokosa masomo.

 Hayo yamesemwa leo Jumatano Novemba 8, 2022 na Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), David Silinde wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Santiel Kirumba.

Katika swali lake la nyongeza, Santiel amesema kwa kuwa wanafunzi wengi wa kike wamekuwa wakikosa masomo kwa siku 50 kwa mwaka.

Alihoji ni nini ahadi ya Serikali katika madarasa mapya ambayo mengi hayana vumba vya kujisitiri.

Akijibu swali hilo, Silinde amesema lengo la kujenga vyumba hivyo ni kuwasaidia wanafunzi hao wanapokuwa katika siku zao za hedhi ili wasikose masomo.

“Tunazielekeza halmashauri zote kujenga vyumba ambavyo vitawasaidia hawa watoto kujisitiri wakati wa hedhi, lengo ni kuhakikisha hawakosi masomo wakati huo ili kuweza kuwasaidia kama ambavyo katika michoro yetu mipya tumeainisha,”amesema.

Katika swali la msingi, Santiel amehoji Serikali haioni haja ya kujenga vyoo maalum kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika madarasa mapya yanayojengwa ili wanafunzi hawa wasikose masomo pindi wanapokuwa kwenye siku zao.

Akijibu swali hilo, Silinde amesema ujenzi wa matundu ya vyoo unazingatia mahitaji ya wanafunzi wote wakiwemo wavulana na wasichana pamoja na wanafunzi wenye mahitaji maalum.

“Itaendelea kuzisimamia na kuzielekeza mamlaka za Serikali za mitaa pindi wanapojenga shule mpya wazingatie kujenga matundu ya vyoo kulingana na michoro na ramani zote zinazotumwa kwao kwa kuwa ndani ya michoro hiyo imejumuisha chumba maalum cha wasichana kwa ajili ya kujisetiri wanapokuwa katika hedhi,”amesema.