Serikali yaagiza uchunguzi upotevu wa dawa Hospitali ya Babati

Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange akizungumza na uongozi wa hospitali ya Babati mkoani Manyara.
Muktasari:
- Baada ya Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange kubaini mianya ya upotevu wa dawa katika Hospitali ya Babati mkoani Manyara ameagiza uchunguzi maalum wa mifumo katika hospitali hiyo.
Dodoma. Serikali imeagiza kufanyika uchunguzi wa mfumo wa uagizaji, Utunzaji na Utoaji wa dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara baada ya kubaini mianya ya upotevu wa dawa kwenye hospitali hiyo.
Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange wakati akiwa ziara ya kikazi mkoani humo.
“Sijaridhishwa na utunzaji wa takwimu za uagizaji, utunzaji na utoaji wa dawa kwa wagonjwa, vile vile hakuna dawa kwa kiwango kinachotakiwa kwenye bohari ya dawa katika hospitali hii” amesema Dk Dugange katika taarifa iliyotolewa leo Februari 21,2023 na kitengo cha mawasiliano Serikalini cha ofisi hiyo.
Amesema Serikali imeweka utaratibu wa kuagiza dawa, kupokea, kutunza na kutoa dawa kwa wagonjwa lakini taratibu hizo hazifuatwi jambo ambalo linatoa mianya ya wizi katika hospitali hiyo.
Dk Dugange amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa Manyara ndani ya siku saba kuhakikisha anapeleka timu maalumu ya kufanya uchunguzi wa uagizaji, utunzaji na utoaji wa dawa ili hatua stahiki zichukuliwe iwapo itajiridhisha upotevu wa dawa.
Pia, Dk Dugange amebaini uzembe mkubwa katika usimamizi wa ujenzi wa wodi tatu na jengo la kuhifadhi maiti ambapo Serikali ilipeleka Sh750 milioni lakini ipo kwenye akaunti zaidi ya miezi mitatu na hakuna kazi iliyofanyika na kuagiza pia ifikapo Mei 30, 2023 ujenzi huo uwe umekamilika.
Aidha, amemuagiza mganga mkuu wa wilaya kuhakikisha jengo la upasuaji na wodi ya wazazi ambavyo vipo katika hatua za ukamilishaji, kuhakikisha vinakamilika na kuanza kutoa huduma ifikapo Machi 15,2023.
Vilevile Dk Dugange amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) Wilaya ya Babati kufanya upembuzi yakinifu wa barabara inayokwenda katika hospitali ya wilaya ili iweze kutengewa bajeti na kutengenezwa.