Serikali yaandaa kongamano la Tehama DRC

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Hahari, Nape Nnauye

Muktasari:

  • Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema kongamano hilo litakalofanyika DRC Oktoba 18 na  19 katika hotel ya Pullman Grand Koravia, Lubumbashi na kwamba litafunguliwa na Waziri wa Posta, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa DRC.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeandaa kongamano la fursa za ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) nchini Jamhuri ya Kidemokrasi Congo (DRC), ikiwa ni moja ya mikakati ya Serikali kuwawezesha wabunifu nchini kutangaza huduma zao nje ya nchi.

 Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Septemba 26, 2022, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Hahari, Nape Nnauye amesema wamechukua hatua hiyo baada ya kufanya vizuri katika makongamano ya ndani.

“Wizara imeanza kutengeneza mkakati wa kuwawezesha wabunifu wa ndani kujitangaza nje ya nchi baada ya kufanikiwa nchini. Tumeanza na makongamano ya ndani na sasa tunakwenda nje ya nchi. Leo natangaza kongamano la kwanza kufanyika nje ya nchi,” amesema Waziri Nape.

Amesema kongamano hilo litakalofanyika nchini DRC Oktoba 18 na 19 katika hotel ya Pullman Grand Koravia, Lubumbashi na kwamba litafunguliwa na Waziri wa Posta, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Nape amesema katika kongamano hilo litakalokuwa na washiriki zaidi ya 300 litakuwa na maonesho zaidi ya 50 ya bidhaa na huduma za Tehema na kwamba wabunifu na wafanyabiashara watapata fursa ya kujitangaza na kushiriki mijadala ya kukuza biashara na huduma zao.

Ameongeza kuwa watashirikiana na kampuni za DRC ambapo pia wataonyesha ubunifu wao na kutafuta fursa za uwekezaji nchini humo.

“Tunataka tuwafungulie njia duniani. Tunaanza na Congo kisha tutakwenda nchi nyingine. Tunataka ku-export (kupeleka) ujuzi wao nje ya mipaka ya Tanzania.

Waziri huyo amesema kuwa wameanzia DRC kwa sababu nchi hiyo pia inakwenda kuunganishwa katika mkongo wa taifa na hivyo kuwa nchi ya nane kuunganishwa na huduma hizo.

“Nawasihi kampuni za Tehema na wabunifu kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kongamano hilo. Tunataka Tanzania ijitanue nje ya mipaka,” amesisitiza Waziri Nape.