Serikali yaanza uchunguzi wanafunzi kufundishwa ulawiti

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari.

Muktasari:

  • Siku chache baada ya gazeti moja kuibua tuhuma za watoto kufundishwa ulawiti mkoani Kilimanjaro, Serikali imeanza uchunguzi wa tuhuma hizo.

Dodoma. Wizara ya Elimu, Sayansi na Elimu ya Juu, imetuma timu maalumu mkoani Kilimanjaro kuchunguza tuhuma za wanafunzi kufundishwa vitendo vya ulawiti katika shule mkoani humo.

 Uamuzi wa Serikali unatokana na gazeti moja nchini kuripoti uwepo wa shule inayofundisha masuala hayo mkoani humo kitendo ambacho ni kinyume na maadili ya Mtanzania.

Akizungumza leo Jumanne Januari 17, 2023 katika viwanja vya Bunge, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema timu hiyo inaongozwa na Kamishna wa Elimu nchini na inajumuisha mwanasheria wa wizara hiyo na mkurugenzi wa udhibiti ubora.

Amesema mbali na hatua hiyo, wamewasiliana na Mkuu wa Mkoa iwapo kuna jinai yoyote ili hatua za kisheria zichukuliwe mara moja katika kukomesha vitendo hivyo.

"Timu imeashaanza uchunguzi katika shule zilizotajwa na hatua za haraka zitachukuliwa kwa wahusika wote watakaobainika kuhusika na kadhia hiyo,” amesema Profesa Mkenda.

Amesema katika kukabiliana na vitendo hivyo, wizara hiyo itatoa namba maalumu kwa ajili ya wananchi kutoa taarifa za vitendo hivyo vinavyochafua taswira ya elimu, kuondoa imani ya wazazi kwa shule na inaaribu vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa.

“Katibu Mkuu atatangaza namba ambayo mtu yeyote akijua kuna vitendo kama hivyo kwenye shule au chuo chochote nasi tutaifanyia kazi kwa kufanya uchunguzi ili kudhibiti vitendo hivyo,” amesema.

Aidha amesema ipo mipango endelevu ya kudhibiti vitendo ambapo wizara yake na inashirikiana na wizara nyingine za kisekta katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsi katika jamii ikiwemo maeneo ya shule na vyuo nchini.