Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yahimiza utunzaji miti baada ya kuipanda

Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, (THBUB) Patience Ntwina (aliyesimama) akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa bustani ya miti eneo jijini Dodoma leo Juni 5, 2026. Picha na Rachel Chibwete

Muktasari:

  • Katibu Tawala Msaidizi Sekta ya Uchumi na Uzalishaji Mali Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba, amesema baadhi ya taasisi zimekuwa na tabia ya kupanda miti na kuitelekeza bila usimamizi wa kutosha, hali inayodhoofisha juhudi za Serikali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Dodoma. Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Dodoma anayeshughulikia Sekta ya Uchumi na Uzalishaji Mali, Aziza Mumba, amezitaka taasisi zinazoshiriki kampeni za upandaji miti kuhakikisha zinaisimamia na kuitunza miti hiyo hadi ikue badala ya kuitelekeza muda mfupi baada ya kuipanda.

Mumba amesema licha ya zaidi ya taasisi 40 kujitokeza kushiriki kampeni za upandaji miti katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma, ni taasisi tatu pekee zilizofanikiwa kusimamia na kuitunza miti hiyo kikamilifu, zikiwemo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Akizungumza leo Ijumaa, Juni 5, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa bustani ya miti eneo la Nkuhungu jijini Dodoma, inayosimamiwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mumba amesema tabia ya kupanda miti bila kuwa na mpango wa kuitunza imekuwa ikikwamisha juhudi za uhifadhi wa mazingira na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

“Kampeni za upandaji miti zimekuwa zikifanyika mara nyingi, lakini miti mingi imeshindwa kukua kutokana na kutelekezwa na taasisi zinazoanzisha kampeni hizo. Ni muhimu kila taasisi inayokuja kuomba eneo la kupanda miti iwe tayari kuitunza hadi itakapokuwa mikubwa,” amesema Mumba.

Amesema changamoto kubwa ni baadhi ya taasisi kuomba maeneo ya kupanda miti bila kuwa na mkakati wa kuhakikisha miti hiyo inatunzwa hadi ikue, jambo linalosababisha miti mingi kukauka muda mfupi baada ya kupandwa.

Mumba ameipongeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kufanikiwa kupanda na kutunza miti 500 katika eneo la Nkuhungu kwa Swai, ambalo awali lilitumika kama kiwanja cha mpira.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa THBUB, Pantience Ntwina, ametoa wito kwa viongozi wa maeneo husika kuongeza ushirikiano katika jitihada za utunzaji wa mazingira pamoja na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Amesema baadhi ya maeneo yanayotekelezwa miradi ya upandaji miti yanakabiliwa na changamoto ya utupaji holela wa taka kutoka majumbani, hali inayosababisha kuziba kwa mitaro na kuharibu mimea iliyopandwa.

Naye, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Nkasori Sarakikya, amesema utunzaji wa mazingira ni sehemu muhimu ya kulinda haki za binadamu, ikiwemo haki ya kuishi katika mazingira salama na kupata chakula.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia kilimo himilivu, uhifadhi wa vyanzo vya maji na urejeshaji wa uoto wa asili katika maeneo yaliyoathiriwa na uharibifu wa mazingira, sambamba na utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

“Tutakuwa na mazingira safi na salama kupitia utoaji wa elimu, urejeshaji wa uoto wa asili na kampeni za upandaji miti ya matunda na vivuli ili kupunguza joto na kujenga mazingira bora ya usimamizi wa haki za binadamu,” amesema Sarakikya.