Serikali yahimiza wanafunzi kushiriki uandishi wa insha
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe.
Muktasari:
- Washindi wa mashindano ya kuandika insha katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekabidhiwa tuzo zao na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia huku Serikali ikitaka ushiriki zaidi.
Dodoma. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe amewataka walimu kuwashawishi wanafunzi kushiriki kwa wingi mashindano ya uandishi wa insha ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Profesa Mdoe ameyasema hayo leo Jumamosi, Julai 15, 2023 wakati wa ugawaji wa zawadi kwa washindi wa mashindano ya uandishi wa insha za SADC na EAC.
Amesema mashindano hayo yamewapa nafasi ya kujifunza zaidi masuala yanayowiana na jumuiya za Sadc na EAC.
“Ili kuandika insha hizo ni lazima wafanye utafiti kwanza na kwa kufanya hivyo wanajifunza kwa vitendo wakati wa wanapokuwa wakiziandika,” amesema.
Amehoji sababu za washiriki wanafunzi kuwa wachache wakati ni sehemu ya mafunzo ambayo pia huwajengea wigo mpana wa uelewa na huwafanya wafaulu vizuri kwenye mitihani yao.
Awali, mratibu wa mashindano hayo, Magdalena Mmbando amesema jumla ya wanafunzi 133 walishiriki uandishi wa insha katika jumuiya ya Sadc ambapo baada ya mchakato wa usahihishaji wakapatikana wanafunzi 10 ambao ni washindi wa kitaifa.
Kwa upande wa mashindano ya EAC, amesema wanafunzi 315 walishiriki katika mashindano hayo na baada ya kusahihisha walipatikana washindi 10.
“Natoa wito kwa walimu na wazazi kuzidi kuwahimiza wanafunzi kushiriki katika mashindano haya na mengine yatakayojitokeza kwani uzoefu unaonyesha huwa wanafanya vizuri katika mitihani ya kuhitimu elimu ya sekondari,” amesema.
Washindi hao walipata zawadi ya fedha taslimu na vyeti huku shule wanazotoka zikipatiwa zawadi ya mashine za kudurufia.