Serikali yaikemea Tanesco nguzo za nje

Muktasari:

Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Uledi Mussa alipotembea Kiwanda cha Tanwat kilichopo mkoani Njombe na kukuta uzalishaji mkubwa wa nguzo imara za umeme, lakini zinauzwa nchi za nje hususan Kenya na Afrika Kusini.

Njombe. Shirika la Umeme nchini (Tanesco) limetakiwa kuacha kasumba ya kutumia mabilioni ya fedha kununua nguzo za umeme nje ya nchi, badala yake linunue ndani ya nchi kwa kampuni za kizalendo ambazo zinazalisha nguzo imara.

Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Uledi Mussa alipotembea Kiwanda cha Tanwat kilichopo mkoani Njombe na kukuta uzalishaji mkubwa wa nguzo imara za umeme, lakini zinauzwa nchi za nje hususan Kenya na Afrika Kusini.

Mussa alishangaa kusikia kwamba kila mwaka kampuni hiyo imekuwa ikiomba zabuni za kuiuzia nguzo Tanesco lakini imekuwa ikinyimwa, licha ya uwekezaji na uzalishaji mkubwa uliopo ambao unatosheleza mahitaji ya shirika hilo na kubaki.

Kutokana na taarifa hiyo, alisema atatumia mamlaka aliyonayo kukutana na viongozi wa Tanesco na kuwaagiza watembelee kiwanda hicho ili wajionee uzalishaji wa nguzo uliopo.

“Tanwat wana uwezo mkubwa wa kuzalisha nguzo kuliko hata hizo kampuni tatu zilizopewa zabuni ya kuiuzia nguzo Tanesco. Nitakutana na menejimenti ya Tanesco waje hapa wajionee ili waache kununua nguzo kwa mazoea, hapa kuna nguzo bora na imara kuliko hata huko Afrika Kusini wanakokimbilia kununua,” alisema Mussa.

Kauli hiyo inakuja siku chache baada ya gazeti hili kuandika taarifa za shirika hilo kuwa katika mchakato wa kununua nguzo 700,000 kutoka Afrika Kusini, hatua iliyotetewa na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchesmi Mramba kuwa inatokana na mahitaji ya sheria ya ununuzi wa umma inayoweka ukomo wa zabuni kutangazwa kimataifa.

Mussa aliitaka Tanesco kutumia fedha ilizonazo katika bajeti ili kununua nguzo katika kampuni hiyo, ikiwa ni njia mojawapo ya kuunga mkono wawekezaji wa ndani na kufanikisha kaulimbiu ya Rais John Magufuli ya kuwa na Tanzania ya viwanda pamoja na kupanua wigo wa ajira kwa Watanzania.

“Tatizo la Tanesco wanatoa zabuni wakiwa wamekaa ofisini, hawaendi kuangalia kwamba huyu anayeomba tenda ana uwezo, ndiyo maana Tanwat wanakosa, lakini Tanwat huyuhuyu Kenya ana uzoefu, ni jambo la kushangaza sana,” alisema Mussa.

Meneja Misitu wa Tanwat, Antery Kiwale alisema tangu kampuni hiyo ianze kuzalisha nguzo imekuwa ikiomba zabuni Tanesco lakini mara zote haipewi, badala yake wamekuwa wakiziuza nchini Kenya na Afrika Kusini ambako Tanesco hukimbilia kununua.

Alisema licha ya uwezo walio nao katika uzalishaji wa nguzo wanashangaa kuona Tanesco inashindwa kuthamini kampuni za kizalendo kwa kuzipa zabuni, badala ya kukimbilia nje.