Serikali yaikosoa taarifa ya KLM kusitisha safari Tanzania

Muktasari:

  • Serikali imekanusha taarifa iliyotolewa na shirika la ndege la Uholanzi (KLM) ya kuwepo kwa hali ya hatari nchini, ikitaka wananchi na jumuiya ya kimataifa waipuuze. 

Dar es Salaam. Serikali imeeleza kusikitishwa na taarifa iliyotolewa na shirika la ndege la Uholanzi (KLM) ya kuwepo kwa hali ya hatari nchini na kusitisha safari zake zilizopangwa kufanyika Dar es Salaam na Kilimanjaro. 

Katika taarifa iliyotolewa katika tovuti ya KLM Januari 27, shirika hilo limewatahadharisha abiria wake na kueleza kusitisha safari katika viwanja vya ndege vya kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA). 

Taarifa iliyotolewa leo Januari 28, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amekanusha taarifa hizo akisema hazina msingi. 

“Taarifa hii haina msingi, haina mashiko, haijali na haina umuhimu na imesababisha hofu isiyo na sababu na kiwewe kwa wananchi na sekta ya anga kwa ujumla. Umma unaaswa kuipuuza hiyo taarifa,” imesema taarifa hiyo. 

Imeendelea, “Wizara inapenda kuufahamisha umma na jumuiya ya kimataifa kuwa, operesheni katika viwanja vya JNIA na KIA zinaendelea. Januari 27, 2023 katika uwanja wa JNIA, ratiba za ndege 17 kati ya 18 zikiwa na abiria 2,545 zimenufaika wakati katika uwanja wa ndege wa KIA, ndege tano zikiwa na abiria 823 zimefanikisha safari zake4. 
“Hadi leo saa 9:15 alasiri leo, safari za ndege za kimataifa 12 zimefanyika.”