Mwili wa Mtanzania aliyefia vitani Ukraine wazikwa Mbeya

Jeneza lililobeba mwili wa Nemes Tarimo likiwa nyumbani kwao Mbezi kwa ajili ya heshima za mwisho. Picha na Hellen Hartley.

Muktasari:

  • Mwili wa Nemes Tarimo aliyefariki dunia katika vita baina ya Urusi na Ukraine umezikwa leo Kijiji cha Kisyeto, Kata ya Msasani, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.

Dar es Salaam. Mwili wa Nemes Tarimo aliyefariki dunia katika vita baina ya Urusi na Ukraine umezikwa leo Kijiji cha Kisyeto, Kata ya Msasani, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.
Nemes aliyekuwa akisoma nchini Urusi aliuawa Oktoba 24, 2022 wakati akiwa vitani Ukraine akipigana kuisaidia Urusi kupitia Kundi la Wagner.
Mwili wa Nemes uliwasili nchini usiku wa Januari 26, 2023 na kupokewa na ndugu zake kisha kupelekwa kuhifadhiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Shughuli ya kuaga mwili wa marehemu ilifanyika nyumbani kwao Mbezi kwa Mzungu jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa jana kwenda mkoani Mbeya.

Awali, akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Januari 25, 2023 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax alisema Tarimo kabla ya kufikwa na mauti, alikuwa vitani baada ya kuwa amejiunga na kikundi cha kijeshi cha kujitegemea cha Wagner ikiwa ni ahadi ya kujinasua kifungoni.

Kaburi la Nemes Tarimo aliyefariki dunia katika vita baina ya Urusi na Ukraine.

Wakati akitolea ufafanuzi Dk Tax alikiri kuwa Tarimo alikwenda Urusi na kujiunga na Chuo Kikuu cha Moscow Technological University (MIREA) mwaka 2020 kwa masomo ya shahada ya uzamili katika fani ya Biashara na Uchakataji wa Taarifa (Business Informatics).

Alisema Machi 2022, Mtanzania huyo alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa mujibu wa Sheria za Urusi kwa vitendo vya uhalifu ambavyo hakuvitaja.

Waziri alisema wizara yake imepokea taarifa kutoka Serikali ya Urusi kwamba akiwa gerezani, Tarimo alipewa nafasi ya kujiunga na kikundi hicho cha kijeshi cha Urusi kiitwacho Wagner, kwa ahadi ya kulipwa fedha na kuachiwa huru baada ya kumaliza muda wa kutumika kwenye vita hivyo.
Alisema baada ya mazungumzo hayo, Tarimo alikubali kujiunga na kikundi hicho na hatimaye alielekea vitani nchini Ukraine hadi alipofikwa na umauti Oktoba 24, 2023.