Mwili wa Mtanzania aliyefia vitani Urusi wawasili nchini

Waombolezaji wakisubiri mwili wa Nemes Tarimo kwa ajili ya maziko nyumbani kwao Mbezi Kwa Mzungu, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mwili wa Mtanzania, Nemes Tarimo  aliyefia nchini Ukraine umewasilini nchini leo Ijumaa Saa 10 alfajiri.

Nemes alifia vitani akiitetea Urusi Oktoba mwaka 2022, baada ya kujiunga na Kikosi cha Wagner kinachomilikiwa na Yevgeny Prigozhin ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais wa nchini hiyo Vladmiri Putin.

Hata hivyo baba yake mdogo, Dickson Tarimo amethibitisha kuwasili kwa mwili wa marehemu Tarimo (33) na kueleza kwamba umepelekwa moja kwa moja Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kuhifadhiwa.

"Mwili umeshafika ila umepelekwa Muhimbili kuwekwa sawa baada ya safari ndefu na baadaye utawasili hapa nyumbani kufanyiwa ibada kabla ya kusafirishwa kwenda Mbeya kuzikwa," amesema Dickson.

Naye Salome Kisale, Dada wa Nemes amesema maandalizi mengine yanaendelea hapa nyumbani huku wakiendelea kuomboleza msiba msiba huo.

Ndugu jamaa, marafiki ikiwemo wanachama na makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanaendelea kuomboleza msiba huo katika nyumba ya familia iliyopo Mbezi Kwa Mzungu, Dar es Salaam.