Siri zaidi Mtanzania aliyefia Russia

New Content Item (1)


Muktasari:

  • Siku nne baada ya familia ya Nemes Tarimo (33), Mtanzania aliyefariki dunia vitani Russia kuitaka Serikali kueleza undani wa kifo hicho, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax jana alijitokeza na kueleza kisa na mkasa hadi mauti yakamkuta.

Dar es Salaam. Siku nne baada ya familia ya Nemes Tarimo (33), Mtanzania aliyefariki dunia vitani Russia kuitaka Serikali kueleza undani wa kifo hicho, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax jana alijitokeza na kueleza kisa na mkasa hadi mauti yakamkuta.

Waziri Tax akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, alisema Tarimo kabla ya kufikwa na mauti, alikuwa vitani baada ya kuwa amejiunga na kikundi cha kijeshi cha Russia, Wagner ikiwa ni ahadi ya kujinasua kifungoni.

Alisema tayari mwili wake umesafirishwa jana kutoka Russia kuja Tanzania kwa ajili ya taratibu za mazishi yatakayofanywa na familia yake na kuwa Serikali inaendelea kuwasiliana kwa karibu na Serikali ya Russia.

Januari 20, akizungumza na Mwananchi nyumbani kwao, dada wa marehemu, Salome Kisale alisema familia inaiomba Serikali kutoa tamko ili kujua kijana wao amekufa kwa sababu gani na kama alikuwa hasomi, yale mambo yaliyokuwa yakiandikwa kwenye mitandao yana ukweli gani.

“Tunaomba Serikali itusaidie kutoa tamko kuwa kijana wetu ni kweli amekufa na chanzo kinachosemekana kina ukweli gani ili tuwe tunaelewa, hivi sasa tunachanganyikiwa, taarifa ni nyingi sana,” alisema Kisale.

“Sisi tunafahamu mdogo wetu alienda Russia mwaka 2016 kwa ajili ya kusoma, lakini baada ya kutangazwa kwa kifo chake ndipo tunapoona kuwa amefariki kama mwanajeshi.”


Ufafanuzi wa waziri

Akizungumzia hilo, Dk Tax alikiri kuwa Tarimo alikwenda Russia na kujiunga na Chuo Kikuu cha Moscow Technological University (MIREA) mwaka 2020 kwa masomo ya shahada ya uzamili katika fani ya Biashara na Uchakataji wa Taarifa (Business Informatics).

Alisema taarifa walizonazo, Tarimo aliuawa Oktoba 24, 2022 na alikuwa amejiunga na kikundi cha kijeshi kwa ajili ya kuisaidia Russia kwenye vita kati yake na Ukraine iliyoanza Februari, 2022.

Alisema Machi 2022, Mtanzania huyo alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa mujibu wa Sheria za Russia kwa vitendo vya uhalifu ambavyo hakuvitaja.

Waziri alisema wizara yake imepokea taarifa kutoka Serikali ya Russia kwamba akiwa gerezani, Tarimo alipewa nafasi ya kujiunga na kikundi hicho cha kijeshi cha Russia kiitwacho Wagner, kwa ahadi ya kulipwa fedha na kuachiwa huru baada ya kumaliza muda wa kutumika kwenye vita hivyo.

Alisema baada ya mazungumzo hayo, Tarimo alikubali kujiunga na kikundi hicho na hatimaye alielekea vitani nchini Ukraine hadi alipofikwa na umauti Oktoba 24, 2023.

Hata hivyo, Waziri Tax alisema ni kosa kwa Mtanzania kujiunga na jeshi lolote awapo nje ya nchi.

“Ikumbukwe kwamba, kwa mujibu wa sheria zetu, Mtanzania yeyote haruhusiwi kujiunga na jeshi la nchi yoyote isipokuwa la Tanzania tu. Hivyo, nitoe rai kwa Watanzania wote kuhakikisha wanazingatia sheria za nchi yetu, kanuni na taratibu zilizopo.

“Napenda kuuhakikishia umma na diaspora wa Kitanzania, wakiwamo wanafunzi walioko masomoni nchini Russia kuwa, Serikali kupitia Ubalozi wake uliopo Russia itaendelea kuwapatia ushirikiano na kuhakikisha Watanzania hao wako salama wakati wote,” alisema Dk Tax.

Waziri Tax alisema Serikali itahakikisha mwili wa Mtanzania huyo unarejeshwa nchini kwa ajili ya kuzikwa na familia yake na kuwa tayari mwili huo ulishaondoka Russia jana asubuhi kuja nchini.

“Wizara inaendelea kuwasiliana na Serikali ya Russia kuhakikisha mwili wa marehemu Tarimo unarejeshwa nchini na kukabidhiwa kwa familia husika ili utaratibu wa mazishi ufanyike kwa kuzingatia mila na desturi za Kitanzania,” alisema.

Alisema Serikali inatoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu na jamaa na Watanzania kwa ujumla kwa msiba huo.

Lakini aliwataka Watanzania kuwa mabalozi wazuri wa kulinda taswira ya nchi wawapo ugenini.

Kwa mujibu wa gazeti la The Moscow Times la Russia, mapema Januari mwaka huu, wafungwa wa kwanza walioandikishwa na kikundi cha kijeshi cha Wagner kutoka jela za nchi hiyo, walimaliza kazi yao ya miezi sita nchini Ukraine na kupokea msamaha walioahidiwa kutoka kwa Serikali ya Russia.

Ripoti za vyombo vya habari zilimnukuu mwanzilishi wa Wagner, Yevgeny Prigozhin akisema:

“Walimaliza mkataba wao. Walifanya kazi kwa heshima, kwa utu. Walikuwa mstari wa mbele. Hakuna mtu mwingine katika ulimwengu huu anayefanya kazi kwa bidii kama walivyofanya.”

Na inaelezwa wapiganaji wengi waliosamehewa, kwa kawaida wanapenda kurudi kwenye jeshi hilo la Wagner kufanya kazi kwa mkataba.