Waziri Tax afafanua Mtanzania aliyefia Ukraine, mwili wasafirishwa kuja nchini

New Content Item (1)


Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax amesema mwili wa Mtanzania aliyefariki dunia vitani nchini Ukraine, Nemes Tarimo umeondoka Urusi kuja nchini kwa ajili ya maziko.

Tarimo aliuawa Oktoba 24, 2022 wakati akiwa vitani Ukraine akipigana kuisaidia Urusi ambayo ilivamia nchi huyo tangu Februari 2022.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Januari 24, 2023, Dk Tax amesema serikali itahakikisha mwili wa Mtanzania huyo unarejeshwa nchini kwa ajili ya kuzikwa na familia yake.

"Wizara inaendelea kuwasiliana na Serikali ya Urusi kuhakikisha mwili wa marehemu Tarimo unarejeshwa nchini na kukabidhiwa kwa familia husika ili taratibu za mazishi ziweze kufanyika kwa kuzingatia mila na desturi za Kitanzania. Mwili umeondoka Urusi asubuhi hii," amesema Dk Tax.

Waziri Tax amesema Tarimo alikwenda Urusi na kujiunga na Chuo Kikuu cha Moscow Technological University (MIREA) mwaka 2020 kwa masomo ya shahada ya uzamili katika fani ya Business Informatics.

Amesema Machi 2022, Mtanzania huyo alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa mujibu wa Sheria za Urusi kwa vitendo vya uhalifu.

Waziri huyo amesema wizara yake imepokea taarifa kutoka serikali ya Urusi kuwa akiwa gerezani, Tarimo alipewa nafasi ya kujiunga na kikundi cha kijeshi cha Urusi kiitwacho Wagner kwa ahadi ya kulipwa fedha na kuachiwa huru baada ya kumalizika kwa vita hiyo.

Amesema Tarimo alikubali kujiunga na kikundi hicho na kwenda vitani nchini Ukraine hadi alipofikwa na umauti Oktoba 24, 2023.

"Ikumbukwe kwamba kwa mujibu wa Sheria zetu, Mtanzania yeyote haruhusiwi kujiunga na jeshi la nchi yoyote isipokuwa Jeshi la Tanzania. Hivyo, nitoe rai kwa Watanzania wote kuhakikisha wanazingatia sheria za nchi yetu, kanuni na taratibu zilizopo.

"Napenda kuuhakikishia umma pamoja na diaspora wa Kitanzania ikiwemo wanafunzi walioko masomoni nchini Urusi kuwa Serikali kupitia ubalozi wake uliopo Urusi itaendelea kuwapa ushirikiano na kuhakikisha Watanzania hao wako salama wakati wote," amesema Dk Tax.