Sintofahamu ya Mtanzania aliyefia vitani akiitetea Russia

Mwanafunzi wa kitanzania, Raymond Tarimo akiwa nchini Urusi enzi za uhai wake. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Familia hiyo imelieleza gazeti hili kuwa, wanaona vitu vingi mtandaoni kuhusiana na kifo cha ndugu yao, lakini hawajapata taarifa rasmi kutoka serikalini au ubalozini inayoeleza sababu hasa za kifo cha kijana wao.

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na taarifa kuwa Mtanzania aliyefia nchini Russia, Nemes Tarimo (33), alikuwa amejiunga na vikosi vya jeshi la nchi hiyo vinavyopambana na majeshi ya Ukraine, familia yake imeiomba Serikali kueleza undani wa kifo chake.

Hata hivyo, juhudi za kupata taarifa za Serikali kuhusu suala hilo hazikuzaa matunda, licha ya ofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Sheiba Bullu kupokea simu na kuahidi kutoa taarifa, hakutoa taarifa hiyo na hakupokea tena simu kila alipopigiwa.

“Nipe muda, tunaandaa taarifa kuhusiana na suala hilo,” alisema Bullu.

Wakizungumza jana na Mwananchi nyumbani kwao Mbezi kwa Msuguri, baadhi ya wanafamilia walisema walipata taarifa ya kufariki kwa ndugu yao Oktoba 2022 kwa marafiki na baadaye walipata taarifa rasmi kutoka Ubalozi wa Tanzania Russia.

Salome Kisale, dada wa Nemes alisema “Nemes alikwenda Russia kwa ajili ya masomo ya shahada ya uzamili katika Chuo cha Teknolojia cha Russia (MIREA), lakini taarifa nyingi mitandaoni zinasema kwamba alikuwa amefungwa na alitokea gerezani kwenda kujiunga na vita.

“Sisi hatujui chochote, isipokuwa tunaiomba Serikali kutoa tamko kuhusu sababu za kifo cha ndugu yetu,” alisema Salome.

Aliendelea kusema kuwa licha ya kupata taarifa hizo, Desemba 2022 waliona video zilizosambaa mitandaoni zikimuonyesha Mtanzania huyo akipewa heshima za kijeshi.

“Ila ilipofika Januari, 2023 ndipo tulipothibitisha kuwa amefariki, lakini chanzo cha kifo bado hatujakifahamu.

“Mwili haujafika, ubalozi pia haukutueleza sababu za kifo chake isipokuwa tulielezwa amefariki lakini mambo ni mengi kwenye mitandao, tunasubiri Serikali ituambie yanayosambaa kama ni kweli,” alisema.

Alisisitiza kuwa kama familia wapo gizani, kwanza walikuwa wanajua amekwenda huko masomoni, kisha wamepata taarifa amefariki, mara alijiunga na jeshi, video zikionekana mtandaoni anaagwa kijeshi. “Kwa kweli haya mambo yanatuchanganya, tunahitaji kauli ya Serikali tujue sababu za kifo chake ni nini.”

Salome alisema Nemes mwaka 2020 alifika nchini kwa mara ya mwisho kwenye sherehe ya kuvishwa pete ya uchumba dada yake na Septemba 18, 2022 waliwasiliana kwa simu akiwa Russia.

Wamzungumzia

Salome alisema Nemes alikuwa kijana mpole sana, lakini mchangamfu kiasi na kwa kweli alikuwa na msaada mkubwa kwa familia, pia alikuwa mtu wa dini na alipenda kujiendeleza.

“Alisoma shule ya Sekondari Tosamaganga iliyopo mkoani Iringa, kisha akajiunga na masomo ya chuo kikuu akisomea shahada ya teknolojia.

“Alifanya kazi katika mashirika mbalimbali kabla ya kupata fursa ya kujiendeleza kimasomo nchini Russia,” alisema.

Kwa mujibu wa familia yake, Nemes alizaliwa mwaka 1989 na alikuwa mtoto wa pekee kwa mama yake aliyefariki 2006 na mpaka anafikwa na umauti alikuwa hajaoa wala hakuwa na familia.

“Taratibu nyingine zinaendelea hapa nyumbani, ila mengine tutaelezwa na ubalozi anakuja lini na atakuja kwa ndege gani,” alisema Christina Keja, ambaye ni shangazi wa marehemu Nemes.

Naye mama mdogo wa Nemes, Royida Sambulika alisema: “Nemes alikuwa kijana mpole asiyependa makundi, alikuwa muda wote anapenda kutumia kompyuta yake na kufanya mambo yake mwenyewe”.