Familia ya Mtanzania aliyefia Russia waiangukia Serikali

Muktasari:

  • Kufuatia taarifa za kifo cha Nemes Tarimo aliyefia nchini Russia, familia yake imekumbwa na sintofahamu ya kifo hicho, wakiiomba Serikali ieleze undani wake, kwani tangu Desemba16, 2022 walikuwa wakifuatilia bila majibu.

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na taarifa kuwa Mtanzania aliyefia nchini Russia, Nemes Tarimo, alikuwa amejiunga na vikosi vya jeshi la nchi hiyo vinavyopambana na majeshi ya Ukraine, familia yake imeiomba Serikali kueleza undani wa kifo hicho.

Nemes aliyekuwa akisoma nchini Russia anadaiwa kufariki Desemba 2022, huku baadhi ya video zilizosambaa mitandaoni zikionyesha Mtanzania huyo akipewa heshima za kijeshi.
Mwananchi limefika nyumbani kwa familia ya Nemes, Mbezi kwa Msuguri jijini hapa na kukuta wanandugu wakiwa wamekusanyika, wakisema wanasubiri taarifa ya Serikali.

“Sisi tunafahamu kuwa mdogo wetu alienda Russia kuanzia mwaka 2016 kwa ajili ya kusoma lakini baada ya kutangazwa kwa kifo chake ndipo tunapoona kuwa amefariki kama mwanajeshi,” amesema dada wa marehemu, Salome Kisale.

Amesema kuwa taarifa sababu za kifo cha mdogo wake zinazoendelea kwenye mitandao wao hawazifahamu.

Salome amesema awali walipokea taarifa za kifo cha Nemes Desemba16, 2022.

“Taarifa za kifo cha Nemes tumezipokea, lakini hatukutaka kuzisema kwanza kwa sababu tulitaka kujua kama ni kweli.

“Ila ilipofika Januari, 2023 ndipo tulipo thibitisha kuwa amefariki lakini chanzo cha kifo bado hatujakifahamu,” amesema.

Hata hivyo, wamesema kuwa bado mwili wa marehemu haujafika na kwamba wanaiomba Serikali kutoa tamko ili kujua kuwa kijana wao amekufa kwa nini na kama alikuwa hasomi je ni kweli yanayoendelea kwenye mitandao?”

“Tunaomba Serikali itusaidie kutoa tamko kuwa kijana wetu ni kweli amefariki na chanzo kinachosemekana ni kweli ili tuwe tunaelewa sababu tunachanganyikiwa taarifa ni nyingi sana,” amesema.

Naye mama mdogo wa Nemes, Royida Sambulika amesema Nemes alikuwa mtoto pekee katika familia yao, aliyekuwa akilelewa na baba pamoja na ndugu wengine baada ya mama yake kufariki mwaka 2006.

“Nemes alikuwa kijana mpole asiyependa makundi alikuwa muda wote anapenda kutumia kompyuta yake na kufanya mambo yake mwenyewe,” amesema.

Juhudi za kutafuta kauli ya Serikali zinaendelea.