Mtanzania aliyefia vitani akitetea Urusi aagwa, aacha mtoto mmoja

Jeneza lililobeba mwili wa Nemes Tarimo likiwa nyumbani kwao Mbezi kwa ajili ya heshima za mwisho. Picha na Hellen Hartley.

Muktasari:

  • Mwili wa Nemes umeagwa leo Januari 27, 2023 Jijini Dar es Salaam baada ya kuwasili kutoka Urusi na utasafirishwa kwenda kuzikwa Tukuyu, Mbeya.

Dar es Salam. Mtanzania aliyefia vitani nchini Ukraine Nemes Tarimo (33), ameacha mtoto mmoja wa kike.

Hayo yamebainika leo Januari 27, 2023 wakati mmoja wa wanafamilia hiyo, Don Ethinic wakati akisoma risala baada ya kumalizika ibada ya kuaga mwili wa ndugu yao.

Ethinic amesema ndugu yao Nemes akiwa Urusi alikoenda kimasomo tangu mwaka 2016 alifanikiwa kupata mchumba ambaye ni Mzungu na kuzaa naye mtoto mmoja wa kike.

"Mtoto huyo anaumri wa miaka mitatu anaishi huko Russia pamoja na mamaake na amepewa jina la mama yake Nemes Lucy," amesema

Mwili wa Nemes aliyefia vitani tangu Oktoba 24,2022 uliwasili alfajiri ya kuamkia leo Januari27, 2023 nchini kutokea Russia na kufanyiwa ibada nyumbani kwake Mbezi kwa Mzungu, Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kwenda Tukuyu mkoani Mbeya ambako unatarajiwa kuzikwa keshoJanuari 28,2023 (Jumamosi).

Hata hivyo, watu wengi waliojitokeza kuomboleza msiba huo hawakupata fursa ya kuona mwili kama ulivyozoeleka utamaduni wa Wakristo bali waliaga kwa kuangalia picha huku ndugu zake wakieleza ulikuwa umeharibika.

Mmoja wa ndugu wa marehemu huyo ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema "Wakati tunakabidhiwa mwili na kuukagua tulibaini mwili ulikuwa nusu (kiwiliwili cha juu) inayoonesha ndugu yetu alifariki kwa kupigwa bomu".

 Alisema hata baada ya kufungwa, taarifa walipata na wanafamilia hao walitafutwa, akiomba msaada lakini alisubiri bila mafanikio kutokana na mvutano uliokuwa unaendelea ndani ya wafamilia ya Nemes.

"Wakati familia ikiendelea kuvutana ndipo alipata ofa akiwa gerezani kwamba aende vitani na baada ya miezi sita ataachiwa huru naye alikubali akajikomboe mwenyewe,"amesema.

Kwa mujibu wa maelezo ya ndugu huyo alisema shabaha ya Nemes ilikuwa iuzwe nyumba yake hiyo Ili ipatikane fedha ya kwenda kumsaidia kutoka gerezani.