Chadema yamlilia Mtanzania aliyefia vitani akiitetea Russia

Muktasari:

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kada wake, Nemes Tarimo aliyefia vitani nchini Ukraine akitetea masilahi ya Russia, atakumbukwa kwa harakati za kutafuta uhuru, haki na Demokrasia ya Maendeleo ya watu.

Dar es Salaam. Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kada wake, Nemes Tarimo aliyefia vitani nchini Ukraine akitetea masilahi ya Russia, atakumbukwa kwa harakati za kutafuta uhuru, haki na Demokrasia ya Maendeleo ya watu.

Kada huyo alifariki dunia Oktoba mwaka jana, alikuwa mwanachama na kada wa Chadema na mwaka 2020 aliomba nafasi ya kuwania ubunge wa Jimbo la Kibamba na kushika nafasi ya tatu kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya Chadema.

Akizungumza Dar es Salaam kwenye msiba huo, Katibu Mkuu wa (Chadema) John Mnyika amesema Nemes Tarimo 33 ametangulia mbele ya haki akiwa bado mdogo lakini atakumbukwa kwa harakati za kutafuta uhuru, haki, demokrasia ya maendeleo ya watu.

Mnyika amesema taarifa za kifo chake walizipokea Kwa masikitiko makubwa huku akieleza alikuwa na ndoto kubwa za kuja kulisaidia taifa na watu wake.

"Ni sala yangu kuwa mwenyezi Mungu akupe rehema na neema kupata mwanga wa milele na upumzike kwa amani," amesema

Naye Mwenyekiti wa Jimbo la Kibamba, Ernest Mgaya amesema katika mchakato wa kura za maoni kwenye uchaguzi wa 2020,Nemes alileta ushindani mkubwa.

Hata hivyo katika uchaguzi huo Mgaya  alishinda na jina lake  kupitishwa na   Kamati Kuu kuiwakilisha Chadema katika kugombea nafasi ya ubunge.

"Licha ya kwamba Tarimo hakuna kiongozi ndani ya chama lakini tunamtumbua alikuwa mwanachama wetu na tutashiriki shughuli zote za msiba kwa ukaribu na familia,"amesema

Amesema kwakuwa  mwili unaenda kuzikwa Tukuyu mkoani Mbeya ulikozaliwa mama yake mzazi, lakini chama hicho kitatuma wawakilishi kuifariji familia.

"Huo ndiyo utaratibu wetu siku zote mwanachama wetu akipata tatizo huwa tunashiriki na sio kwa huyu Tarimo tu,". amesema

Nemes alifariki Oktoba mwaka jana akiwa vitani nchini Ukraine akitetea masilahi ya Russia baada ya kujiunga na  kikosi cha Wagner kinachomilikiwa na Yevgeny Prigozhin ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais wa Russia Vladmir Putin.