Serikali yajenga jengo la kuhifadhia mazao Buchosa

Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo akizungumuza na wananchi wa Kata ya Nyakasungwa alipotembelea mradi wa kuhifadhia mazao. Picha na Daniel Makaka

What you need to know:

Serikali imekamilisha ujenzi wa jengo lenye uwezo wa kuhifadhi tani 1,500 za mahindi na karanga wilayani Sengerema lililogharimu zaidi ya Sh1 bilioni.

Buchosa. Wananchi wa Halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wameishukuru Serikali kwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa jengo la kuhifadhia mazao ya karanga na mahindi ambao utaepusha mazao hayo kushambuliwa na fangazi wanaoeneza sumu kuvu.

Wananchi hao wa Kata ya Nyakasungwa unapojengwa mradi huo wametoa shukrani hizo leo Alhamis Juni 8, 2023 baada ya Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo kufanya ziara ya kusikiliza kero zao.

Mkazi wa Kijiji cha Nyakasungwa, Juma John amesema ushirikiano wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan na mbunge wao ndiyo chanzo cha maendeleo ya wananchi katika eneo lao.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo ,Mifugo na Uvuvi, Anthony Mbega amesema jengo hilo lililogharimu zaidi ya Sh1 bilioni linauwezo wa kubeba tani 1, 500 za mahindi na karanga kwa wakati mmoja nakuwataka wananchi kitumia fursa hiyo na kuhifadhi mazao yao mahali salama.

Amesema madhara yanayosabishwa na sumu kuvu ni mtu kupata saratani, udumavu kwa binadamu na mifugo ambapo madhara hayo husababisha vifo.

Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo amesema mradi huu utakuwa mkombozi kwa wakulima wa mazao ya mahindi na Karanga ambayo yamekuwa yakishambuliwa na fangazi zinazoeneza ungonjwa wa sumu kuvu.

“Kwa sasa  maendeleo yanapatikana Buchosa hivyo tuendelee kuwaamini wawakilishi wenu waonaopambana usiku na mchana kuwatumikia wananchi,” amesema Shigongo