Serikali yakabidhi bwawa la mifugo Chalinze

Wednesday July 14 2021
serikalipic
By Julieth Ngarabali

Chalinze. Serikali imekabidhi bwawa la maji la Chamakweza kwa uongozi wa Halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani baada ya kukamilisha ukarabati uliogharimu Sh671 .5 milioni kwa lengo la kuhudumia mifugo na kaya zaidi ya 2,500 wa eneo hilo.

Ukarabati wa bwawa hilo umehusisha kuongeza urefu wa tuta, kujenga njia ya maji, kuondoa tope ndani ya bwawa, kujenga kidakia maji kwenda kwenye mabirika ya kunyweshea mifugo, kuweka mfumo wa mabomba na kusambaza maji na kujenga sehemu ya kuchota maji kwa matumizi ya binadamu.

Naibu Waziri wa Mifugo na uvuvi, Abdallah Ulega amekabidhi bwawa hilo mbele ya Mbunge wa jimbo hilo, Ridhiwan Kikwete na kutaka wanakijiji kuunda kamati ya usimamizi wa bwawa hilo na kutaka apelekewe  ripoti ya maboresho kabla ya Julai 16.

Waziri Ulega amesema Serikali imedhamiria kuondoa migogoro ya wafugaji na wakulima kwa kuhakikisha huduma za chanjo, dawa, malisho na maji yanapatikana kwenye maeneo ya wafugaji.

Awali, Mkurugenzi wa huduma za mifugo kutoka Wizara ya mifugo na uvuvi, Profesa Hezron Nonga amesema bwawa hilo litaendelea kuwa chini ya uangalizi wa mkandarasi kwa mwaka moja ili,kukagua mapungufu ya kiufundi yatakayojitokeza.

Profesa Nonga ameeleza kuwa bwawa hilo linauwezo wa kutunza lita milioni 108.16 za ujazo  wa  maji kwa mwaka na hivyo kunywesha ng'ombe 15,431, mbuzi 453, kondoo 2,103 na punda  pamoja na kunufaisha kaya 2,566 za wafugaji wanaoishi vijijini vya jirani .

Advertisement

Kwa upande wake, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete ameishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma za maji jamii hiyo ili kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji.

"Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuhakikisha kero za wafugaji zinaondoka na kuondoa migogoro na wakulima, lakini tunaomba utuongezee mabwawa mengine manne ili kukidhi mahitaji ya wana Chalinze," amesema Ridhiwani

Advertisement