Serikali yakumbushwa ahadi yake kujenga wodi za wagonjwa

Wajumbe wa Kamati Tekelezaji ya UVCCM Wilaya ya Sengerema wakitoa vifaa mbalimba ikiwemo sabuni kwa wagonjwa walipofika Kituo cha Afya Nyamatongo kwa ajili ya kupata huduma. Kamati hiyo ilifika kwenye kituo hicho kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM. Picha na Daniel Makaka

Muktasari:

Serikali imekumbushwa kutimiza ahadi ya ujenzi wa wodi za wagonjwa katika Kituo ya Afya Nyamatongo kilichopo Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza iliyoitoa miaka sita iliyopita.

Sengerema. Serikali imekumbushwa kutimiza ahadi ya ujenzi wa wodi za wagonjwa katika Kituo ya Afya Nyamatongo kilichopo Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza iliyoitoa miaka sita iliyopita.

Akitoa taarifa Juni 2, 2023 mbele ya Kamati Tekelezaji ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Sengerema iliyokuwa ikikagua utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye Kata ya Nyamatongo, Mganga Mkuu wa kituo hicho, Dk Stivin Godwin amesema ahadi hiyo ilitolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipotembelea kituo hicho miaka sita iliyopita.

Dk Godwin amesema wagonjwa 900 hadi 1, 000 wanahudumiwa katika kituo hicho kwa mwezi huku, kwa siku wakihudumiwa wagonjwa 30 hadi 50 ambapo huduma mbalimbali zinatolewa ikiwemo ya tatizo la ugonjwa wa moyo.

Amesema katika kituo hicho kinachoendeshwa na Serikali kwa ubia na Shirika lisilo la kiserikali la Cedar Foundation, wanapata changamoto kubwa wanapopata wagonjwa wanaopaswa kulazwa hivyo wodi zinahitajika.

“Kituo cha Afya Nyamatongo kinahudumia Kata nne  za Nyamatongo, Ngoma, Chifunfu na Katunguru hivyo wagonjwa wanaotoka mbali wanahangaika kutokana na kutokuwa na wodi,” amesema Godwin

Kituo hicho kina sehemu ya kupumzishia kina mama waliojifungua na wangonjwa wengine wa dharura.

Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Sengerema, Patrick Mundeba amewatoa hofu watumishi wa kituo hicho kuwa ahadi zote zilizotolewa na Serikali zitatekelezwa.

Amesema wanatawasilisha ngazi za juu ili ahdi ya iliyotolewa itekelezwe na wananchi waweze kupata huduma huku akiwapongeza watumishi wa kituo hicho kutoa huduma bora kwa wangojwa.

Naye Mjumbe wa UVCCM, Paul Mfumakule amewaomba wananchi wanaopata changamoto ya afya waendee Kituo cha Afya Nyamatongo kutokana na huduma bora zinazotokewa na watumishi wake.