Serikali yamaliza mgogoro wa ardhi Bonde la Usangu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa eneo la Mbalizi Mkoani Mbeya, baada ya kuwasili mkoani humo kwa ziara ya kikazi katika Mikoa ya Mbeya na Songwe Januari 16, 2023

Muktasari:

  • Mgogoro wa ardhi wa bonde hili umedumu kwa muda mrefu kiasi cha kusababisha migogoro ya mara kwa mara baina ya wananchi na uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imemaliza mgogoro wa matumizi ya ardhi wilayani Mbarali mkoani Mbeya ambao umedumu kwa takribani miaka 15.
Mgogoro huo ulihusisha wakazi wa wilaya hiyo hususan wanaoishi eneo la Bonde la Usangu dhidi ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Akizungumza katika kikao na wadau waliowekeza katika Bonde la Usangu jana Januari 16, 2023 mkoani Mbeya, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye Tangazo la Serikali Namba 28, ambayo itawawezesha wananchi kufanya shughuli za kilimo na ufugaji endelevu.
Amesema marekebisho ya tangazo hilo yatawezesha pia baadhi ya vitongoji vilivyokuwa vimetangazwa awali kuwa ndani ya hifadhi, kuachwa nje ya mipaka ikiwemo kutoa eneo la hekta 74,000 kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.
 “Hii GN 28, Serikali tumeamua kuitafutia ufumbuzi baada ya vikao vingi na wadau kwa faraja kabisa, nataka niwaambie tumefikia hatua nzuri itakayowezesha kila anayejishughulisha na kilimo kuendelea na kilimo chake na kila anayejishughulisha na mifugo kuendelea na ufugaji wake.”
Majaliwa amesema Serikali inataka kuhakikisha Wilaya ya Mbarali inaendesha shughuli za kilimo kitaalamu na kwa tija.
“Tumeona maendeleo makubwa na ujenzi wa viwanda vya mtu mmoja mmoja na vikundi, Serikali inataka kuona shughuli hizo zinakuwa endelevu, tunataka mpanue viwanda vyenu na mzalishe zaidi,” amesema waziri mkuu huyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali imeamua kuitoa nje ya hifadhi Ranchi ya Usangu kwa ajili ya shughuli za ufugaji wa kisasa.
“GN namba 28 iliingiza ranchi ndani ya hifadhi, lakini ili wafugaji wawe huru, tumeindoa na hivyo itakuwa nje, tumeacha na mito kadhaa ambayo itahifadhiwa kwa sheria za mazingira,” amesema Majaliwa.
Pia, Majaliwa amewataka wafugaji kujiamini kwa sababu mifugo ni uchumi. “Tunataka tuondokane na uchungaji na kuwafanya Watanzania wafugaji kuacha kutembea umbali mrefu na ng'ombe, hii inaondoa thamani ya nyama, tunataka mfuge kisasa.”
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula amesema maeneo ambayo yameondolewa katika hifadhi, serikali itahakikisha mpango bora wa matumizi ya ardhi unawekwa ili wananchi waweze kufanya kile ambacho kimepangwa kufanyika kwa wakati huo.
Waziri Mabula amesema watahakikisha wananchi hao wanapata hati miliki za maeneo yao ili waweze kuzitumia katika shughuli mbalimbali za maendeleo na mpango wa uandaaji utafanyika kwenye vijiji vyote vinavyohusika.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo amesema kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji watumiaji wote wanapaswa kuheshimu sheria ya mazingira.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana amewataka watumiaji wa eneo lililotolewa kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kilimo waendelee kulilinda eneo lililobaki. “Tusifuge wala kulima katika eneo lililobaki eneo hili ni chanzo kikubwa cha maji na sehemu ya utalii,” amesema Dk Chana.
Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema ranchi ya Usangu ni kwa ajili ya shughuli za ufugaji tu na isitokee yeyote akafanya tofauti na lengo.
“Tulioko kwenye ranchi tufuge, wengine mnabadilisha matumizi wengine hamfugi lakini mnakodisha watu wanakuja kulima kwenye vitalu, wale mnaolima badala ya kufuga tutawanyang’anya vitalu,” amesema Waziri Ndaki.