Serikali yaomba siku 14 kujadiliana na Rhoda

Muktasari:

  • Rhoda anadaiwa kusafirisha kilo 23 za Mirungi, tukio analodaiwa kulitenda Januari 26, 2023 katika mtaa wa Wailes, uliopo Temeke.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu, imetoa siku 14 kwa Serikali kuendelea na majadiliano dhidi ya mshtakiwa Rhoda Salum (48) anakabiliwa na kesi ya kusafirisha kilo 23.84 za dawa za kulevya aina ya Mirungu.

 Mahakama hiyo imefikia hatua hiyo, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha ombi mahakamani hapo, waliomba wapewe siku 14 kwa ajili ya kuendelea kufanya majadiliano na mshtakiwa huyo ili aweze kuimaliza kesi yake.

April mwaka huu, Rhoda, alimuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akiomba kukiri shtaka lake na kupunguziwa adhabu ili aweze kuimaliza kesi hiyo.

Wakili wa Serikali Ashura Mnzava ameieleza mahakama hiyo, leo Oktoba 2, 2023 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

" Mheshiwa hakimu, wenzetu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ( DCEA) wanaomba wapewe wiki mbili ili waweze kuendelea na kikao cha majadiliano ya kuimaliza kesi hii dhidi ya mshtakiwa huyo," amedai Wakili Mnzava.

Hakimu Kabate baada ya kusikiliza hayo, alikubaliana na maombi ya upande wa mashtaka na kuwapa wiki mbili ili waweze kuendelea na majadiliano.

Baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 17, 2023 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka linalomkabili halina dhamana.

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa katika mahakama hapo, Februari 16, 2023 na kusomewa kesi inayomkabili.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 26, 2023 katika Mtaa wa Wailes uliopo Wilaya ya Temeke.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa huyo alikutwa akisafirisha kilo 23 za mirungi, kinyume cha sheria.