Serikali yatakiwa kuongeza kasi ujenzi wa SGR

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini wakiwa katika Picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga walipotembelea kituo Cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme Cha Msamvu Morogoro. Lilian Lucas.

Morogoro. Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imeitaka Serikali kuongeza kasi ya kukamilisha maeneo machache yaliyobaki kwenye ujenzi wa mradi wa Treni ya Mwendo wa haraka (SGR) ili uwekezaji uliofanyika uanze kuonyesha manufaa kwa Taifa na kuanza kazi mara moja.

Aidha kamati hiyo imesema Watanzania wanashauku ya kuona SGR inaanza kufanya kazi na imeitaka Serikali iongeze kasi ya kukamilisha maeneo machache yaliyobakia.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk David Mathayo alisema hayo Novemba 12 Mjini Morogoro wakati wa ziara ya kawaida na ya kikazi kwa ajili ya kukagua  utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa KV 220 kwa ajili ya uendeshaji wa treni ya Mwendokasi (SGR).

Dk Mathayo kupitia Kamati yake, ameeleza kwa namna kamati ilivyofurahishwa na Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kazi ambayo imeonekana katika utekelezaji wa mradi huo mkubwa.

Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umeme itakayowezesha kulisha vituo vinne vya kupoza umeme kwa kiwango cha kuendesha treni hiyo ambapo awamu ya kwanza (SGR lot 1) kutoka Kinyerezi Dar es Salaam hadi Kingolwira mkoani Morogoro yenye urefu wa kilometa 160 katika vituo vya kupoza umeme cha Pugu, Ruvu, Kidugalo na Kingolwira umeshakamilika kwa asilimia 100.

Kamati hiyo imesema wa utekelezaji wa mradi wa awamu ya pili kwa kipande cha kutoka Msamvu hadi Ihumwa ambao kwa  sasa umefikia asilimia 99, iliitaka serikali iendelee kusukuma kasi kwa  Tanesco ikamilishe asilimia moja iliyopakia ya ujenzi  wa  kipande hicho.

“Tunaishauri serikali iongeze speed ili tumalizie huu mradi  na tuendelee na mambo mengine tunataka kuona kwa sasa inafanya kazi, Reli inapitisha vichwa na mabehewa ya abiria na mizigo, tuone uwekezaji tulioufanya una manufaa kwa nchi yetu,”amesema mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Mathayo.

Imeitaka Serikali kuendelea kutoa elimu na tahadhari kwa wananchi kuhusu hatari ya kupitia meneo yaliyozungushiwa uzio na kupitisha mifugo karibu na njia ya Reli ya Mwendokasi ili kuepusha majanga.

“Ni vyema kwa serikali kuu ikishirikiana  na serikali za mitaa kuzidi kutoa elimu ya  tahadhari kwa ajili ya kuzuia ajali ambazo zinaweza kutokea,”amesema.

“Serikali tuwatumie watendaji wa vijiji, kata wenyeviti wa vijiji , mitaa na vitongoji wasaidiane na serikali kuu kuendelea kutoa elimu kwa jamii yetu hasa wananchi wanaopita maeneo ambayo yamewekewa uzio,” amesema.

Naye Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema, wizara chini ya Naibu Waziri Mkuu na waziri wa Nishati , Dk Doto Biteko itaendelea kusimamia miradi ya umeme kwa uaminifu mkubwa .

Kapinga, amesema Serikali imewezesha fedha kiasi cha Sh76.23 bilioni zilizokamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi huo ulikamilika kwa asilimia 100 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

Amesema , serikali pia imetoa  Sh97.5 bilioni kwa awamu ya pili ya mradi huo wenye urefu wa kilometa 416 kutoka Msamvu mkoani Morogoro hadi Kintinku Manyoni na  kazi  inafayika sambamba na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme cha Msamvu Morogoro na Zuzu Dodoma.

Kapinga amesema, awamu hiyo inahusisha ujenzi wa vituo vidogo saba vya kupoza umeme ufikie kiwango cha kutumika kwenye treni  ambavyo ni Mkata , Kidete , Godegode , Igandu, Ihumwa , Kigwe na Kintinku ambapo kipande cha kutoka Msamvu  hadi Ihumwa (SGR Lot 2-1) umefikia asilimia 99 ambao ulianza Oktoba 15, 2020  na unatarajiwa kukamilika Januari 31, 2024.