Serikali yawatoa hofu wafasiri Rukwa

Rukwa. Uongozi wa Serikali wilayani Sumbawanga mkoani hapa umewaondoa hofu wakazi wa Manispaa ya Sumbawanga kuhusu kubadilika kwa matumizi ya Stendi Kuu ya Mabasi yaendayo mikoani kutoka stendi ya zamani ya Soko Matola kuelekea Stendi Mpya ya Katumba.

Akizungumza na Mwananchi Digital ofisini kwake leo Novemba 14, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Ally Chirukile amesema stendi zote mbili zitatumika na wapuuze propaganda zinaendelea kuenea kwamba stendi ya zamani ya Soko Matola itafungwa ili ibaki kutumika stendi mpya ya Katumba.

"Kuna mtu amejirekodi na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii akidai mkuu wilaya (mimi) nimeagiza ile stendi ifungwe na abiria wawe wanatumia ile mpya Katumba...hizi taarifa siyo za kweli zinalenga kuleta taharuki kwa watumiaji wa stendi hizo.

Wengine wameingiza siasa kwenye jambo hili wakidai kwamba baadhi ya wakatisha tiketi pale Soko Matola ambao ni makada wa CCM wametishia kurudisha kadi kwa kuwa hawatendewi haki," amesema.

Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza kuwa utaratibu wa awali wa matumizi ya stendi zote mbili utaondelea kufuatwa hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo.

Stendi Kuu ya Mabasi ya Katumba imejengwa kwa kutumia zaidi ya Sh9 bilioni na ipo nje kidogo ya Manispaa ya Sumbawanga umbali wa zaidi ya kilometa 12 kutoka mjini ambapo watumiaji wake wamekuwa wakilalamika kuwa wanatumia gharama kubwa kufika katika stendi.

"Hata mimi nikisikia tunahamishwa hapa stendi nikawaza umbali uliopo wa kuifikia Katumba, nikaona siyo haki wasafiri watakuwa wakipata shida kwenda umbali wote huo...kama zitaendelea kutumika zote mbili ni jambo jema," amesema God Mwanisawa