Sh1.76 bilioni zatengwa kugharamia mapitio mitaala ya elimu

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk Aneth Komba akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 20222 hadi 2023 jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

Wakati shughuli ya ukusanyaji wa maoni kwa ajili ya maboresho ya mitaala ikitarajiwa kukamilika Desemba 2022, Sh1.769 bilioni zimetengwa ili kumalizia majukumu hayo.

Dar es Salaam. Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imesema Sh1.769 bilioni zimetengwa mwaka huu wa fedha 2022/23 ili kumalizia mapitio ya mitaala ya elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu unatarajiwa kukamilika Desemba 2022.

 Fedha hizo zimetengwa ikiwa ni baada ya Sh1.427 bilioni kutumika mwaka 2020/2021 huku takribani wadau 103,210 wakifikiwa katika mikoa tofauti nchini.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Agosti 9, 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa TET, DK Aneth Komba wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Dk Aneth amesema hatua inayofuata katika mwaka huu wa fedha ni kuwashirikisha wadau kuhusu rasimu za mitaala zilizopendekezwa na kuendelea na hatua ya kuandaa vifaa vingine vya utekelezaji mitaala.

“Hii ni pamoja kuandaa muhtasari na kutoa mafunzo ya walimu na wasimamizi wengine wa mitaala,” amesema Dk Komba.

Amesema shughuli ya ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau ni enedelevu na kamati ya kitaifa ya mitaala iliyoteuliwa na waziri wa elimu sayansi na teknolijia, Profesa Adolf Mkenda inaendela kukutana na makundi mbalimbali.


“Na katika siku za hivi karibuni, tunatarajia kukutana na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ili kuweza kupata maoni yao juu ya nini kifanyik,” amesema Dk Komba.

Amesema katika mwaka uliopita, fedha iliyotengwa ilitumika kukusanya maoni ya wadau, kuchakata data na kuandaa rasimu za mitaala ya ngazi zinazopendekezwa.

“Baadhi ya wadau waliofikiwa ni viongozi wa Serikali, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wahitimu wa vyuo vikuu, walimu, wazazi, wanafunzi wa shule a msingi, sekondari, vyuo vya kati na vikuu, mshirika yasiyo ya kiserikali, walimu wakuu, viongozi vyma vya siasa, dini, maofisa elimu mkoa na wilaya, wahadhiri na wakufunzi,” amesema Dk Komba.