Sh1 bilioni kuwapa maji wananchi 5520 Pangani

Meneja wa Wakala wa maji vijijini na usafi wa mazingira ( Ruwasa) mkoani Tanga, Mhandisi Upendo Omari akikagua mradi wa maji wa kijiji cha Kipumbwi kilichopo Wilayani Pangani. Picha na Susan Uhinga

Muktasari:

Zaidi ya Sh1 bilioni zimetuka katika kutekeleza mradi wa maji katika Vijiji vya Kipumbwi na Mlazo vilivyopo Wilaya ya Pangani mkoani Tanga.

Pangani. Zaidi ya Sh1 bilioni zimetuka katika kutekeleza mradi wa maji katika Vijiji vya Kipumbwi na Mlazo vilivyopo Wilaya ya Pangani mkoani Tanga.

Mradi huo unatarajia kuwanufaisha wananchi wapatao 5,520 katika vijiji hivyo ambao walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi jambo lililokuwa likizorotesha shughuli zao za maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa utiaji saini wa utekelezaji wa mradi huo Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini na Usafi wa Mazingira (Ruwasa),  Mhandisi Upendo Omari amesema mradi huo utasaidia kutatua kero iliyokuwa inawakabili wananchi hao kwa muda mrefu.

Amesema mkandarasi amepewa miezi sita kuhakikisha anakamilisha kwani serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi huo kwa lengo la kuwapunguzia adha wananchi hao.

“Tumeshusha zoezi hilo chini kwa wakuu wa wilaya na madiwani kwa kuwa malalamiko yamekuwa mengi katika utekelezaji wa miradi na hasa kwa kutumia fedha za ndani kwani taratibu zimekuwa hazifuatwi,” amesema Mhandisi Upendo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Masaika George Mariano amesema anatamani kuona mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa bila kuwepo kwa visingizio vyovyote ili kuwaondolea kero wananchi hao.

Amesema kumekuwa na changamoto ya wakandarasi wengi kuwa na kazi nyingi na wengine kuwa na mitaji midogo jambo linalosababisha ucheleweshaji katika utekelezaji wa miradi.

“Nasisitiza suala la muda kama tulivyosaini mkataba hapa maana mnakuwa na kazi nyingi mwisho mnashindwa kujigawa matokeo yake miradi ya wananchi inachelewa na sisi viongozi wa kisiasa tunaonekana waongo kwa wapiga kura wetu,” amebainisha diwani huyo.

Naye Mwanaisha Kajembe mkazi wa Kijiji cha Kipumbwi, ameishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kuwafikishia huduma ya maji safi na kwamba kero hiyo imewatesa kwa muda mrefu.

“Tumehangaika mno kupata huduma ya maji hapa kijijini hata shughuli za kiuchumi zinazorota kwa kuwa muda mwingi tunatafuta maji kwa hiyo kukamilika kwa mradi huu tunaamini kwetu itakuwa mkombozi,” amesema Mwanaisha.

Utiaji saini wa mkataba wa utekelezaji wa mradi huo umeshuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Diwani wa Kata ya Masaika , mkandarasi aliyeshinda tenda na Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Omari.