Sh18 bilioni zinahitajika kukarabati miundombinu ya barabara Morogoro

Mwonekano wa sehemu ya  barabara ya Mtimbira kwenda Malinyi iliyokatika  hivyo  magari kushindwa kupita eneo hilo. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  •  Aprili 25, 2024 Mwenge wa Uhuru utapokelewa wilayani Malinyi, lakini hakuna  uhakika kama utaweza kukagua na kuzindua sambamba na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi yote waliyoianisha kutokana na hali mbaya ya barabara.

Morogoro. Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali wilayani Malinyi mkoani  Morogoro, zimesababisha adha kubwa ikiwamo ya usafiri wa mabasi yanayoingia na kutoka kusitisha safari zake.

Mkuu wa wilaya hiyo, Dastan Waryuba amesema hali hiyo inasababisha shughuli nyingi za kiuchumi kusimama.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 23,2024  Waryuba amesema mvua hizo zimesababisha pia kuzorota kwa shughuli katika sekta nyingi ikiwamo ya elimu.

Amesema mpaka sasa shule za msingi Magugila, Kiwale na Lugala zimefungwa  tangu mvua zilipoanza kunyesha na zitafunguliwa maji yakipungua.

Mbio za Mwenge hatihati

Mkuu huyo wa wilaya amesema Aprili 25, 2024 wataupokea Mwenge wa Uhuru, lakini hawana uhakika kama utaweza kukagua na kuzindua sambamba na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi yote waliyoianisha kutokana na hali mbaya ya barabara.

"Kuna maeneo kwa sasa tumeamua kubuni njia mbadala ili Mwenge wa Uhuru upite na kukagua miradi, tunaendelea na ujenzi wa haraka na kuweka vifusi kwenye zile barabara ambazo tunadhani tutapita upite hivyohivyo," amesema Waryuba.

Kutokana na hali hiyo tumeshachukua hatua ya kuwaondoa wananchi kwenye maeneo hatarishi hasa mabondeni kwa kuwa tumeshawapoteza wengi tangu Januari mvua zilipoanza.

"Tangu mvua zianze kwenye halmashauri yetu watu 33 wameshafariki ni wengi ndiyo maana unaona  tuko karibu na wananchi ili kuhakikisha hatupotezi wengine zaidi, licha ya mvua kuendelea kunyesha kwenye maeneo yetu," amesema Waryuba.


Mbunge afunguka

Kwa upande wake Mbunge wa Malinyi, Antipas Mgungusi amesema mvua hizo zimesababisha kukatika kwa mawasiliano baada ya barabara ya kutoka Mtimbira hadi Malinyi kutopitika.

“Zamani nauli ilikuwa Sh22,000 kutoka Ifakara hadi Malinyi lakini kwa sasa imeongezeka mara dufu na wasafiri wanashindwa kumalizia safari zao. Wengine hulazimika kutumia usafiri wa bodaboda na madereva wa boda hujipangia bei watakazo wao,” amesema Mgungusi.

Hata hivyo, amesema baada ya kuwasilisha kilio hicho kwa Serikali tayari hatua mbalimbali zimeshachukuliwa ikiwa ni pamoja na kupeleka timu ya wahandisi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad), walioweka kambi eneo la Mtimbira wakisubiri mvua zipungue ili wafanye marekebisho ya dharura.

"Kutokana na hali mbaya iliyopo sasa upo wasiwasi Mwenge wa Uhuru ukakimbizwa katika kata moja ya Mtimbira, kule Malinyi hakuendeki japokuwa ipo miradi iliyopangwa kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi," amesema mbunge huyo.

Naye Meneja wa Tarura Mkoa wa Morogoro, Emanuel Ndyamukama amesema kutokana na uharibifu wa miundombinu ya barabara, madaraja na makaravati kwa mkoa mzima wa Morogoro, jumla ya Sh18 bilioni zinahitajika kufanya matengenezo na tayari wameshawasilisha bajeti hiyo serikalini.

Ndyamukama amesema Sh2 bilioni zimeshatolewa kwa ajili ya matengenezo kwenye maeneo ambayo hayajaathirika kwa kiwango kikubwa.

 “Kule wilaya ya Malinyi na Kilombero kunahitaji fedha nyingi kwa kuwa uharibifu ni mkubwa na kwa sasa hata tukipata fedha, hatutaweza kufanya matengenezo kwa kuwa mvua kubwa bado zinaendelea kunyesha," amesema Ndyamukama.


Amesema maeneo mengi ya Mkoa wa Morogoro yanayohitaji ukarabati na matengenezo ya miundombinu yake na kwamba kati ya Kilomita 6256.9 za barabara zinazohudumiwa na Tarura kilomita 3,115 zimesombwa na maji na kukatika kabisa.

Kuhusu makaravati, Ndyamukama amesema mkoani humo kuna  jumla ya makaravati 3,500 yanayosimamiwa na kuhudumiwa na Tarura na kati ya hayo 211 yamesombwa na maji.

Mwananchi imezungumza pia na Mkurugenzi wa mabasi ya Alsaedy yanayofanya safari zake kati ya Morogoro na Malinyi, Mbarak Alsaedy ambaye amekiri mabasi yake kusitisha safari za kwenda Malinyi kutokana na ubovu wa barabara.

Amesema tangu wasitishe safari hizo zimeshapita wiki mbili sasa na machache yanayoenda njia hiyo yanaishia Mtimbira.

"Nimeona bora nisitishe safari za Malinyi kwa sasa hadi hali ya barabara itakapokuwa nzuri, nikilazimisha kupeleka mabasi lazima yatakwama nitaendelea kuingiza hasara,”  amesema Mbarak.