Sh19.5 bilioni kuboresha bandari ya Bukoba
Muktasari:
Bandari ya Bukoba inatarajiwa kufanyiwa maboresho ikiwemo kujengwa gati jipya, kuboresha magati yaliyopo, ujenzi wa jengo la abiria, ujenzi wa maegesho ya magari, ujenzi wa miundombinu ya umeme na maji ya mvua itakayogharimu Sh19.5 bilioni.
Bukoba. Bandari ya Bukoba inatarajiwa kufanyiwa maboresho ikiwemo kujengwa gati jipya, kuboresha magati yaliyopo, ujenzi wa jengo la abiria, ujenzi wa maegesho ya magari, ujenzi wa miundombinu ya umeme na maji ya mvua itakayogharimu Sh19.5 bilioni.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 21, 2023; Mkuu wa bandari hiyo, Michael Palangyo amesema ujenzi huo umeanza tangu Februari, 2023 ambao utatumia mwaka mmoja na nusu hadi kukamilika kwake.
“Ujenzi unatarajia kukamilika Julai, 2024 ambapo utatumia Sh19.5 bilioni, hadi sasa ni miezi sita tangu umeanza na mkandarasi ameishafanya kazi takribani kwa asilimia 13,”amesema Palangyo
Amesema ujenzi wa bandari hiyo si tu kwa ajili ya kupokea meli kubwa ya Mv Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’ bali pia ni sehemu ya kuboresha mazingira kwani yamebadilika toka ilipojengwa 1,945 licha ya kuwepo maboresho madogo madogo.
Wakati huo huo, Wajumbe wa Bodi ya Wakala wa Huduma za Meli nchini (Tasac) wametembelea bandari ya Bukoba, Kemondo na kiwanda cha kuchakata minofu ya sangara kilichopo Bukoba.
Mjumbe wa bodi hiyo, King Chiragi amesema lengo la ziara hiyo ni kubaini changamoto zinazokabili usafiri wa majini, kuzitafutia ufumbuzi na mwisho wa siku usafiri huo uwe salama nakufanya bandari na mialo zifanye kazi zao kwa ufanisi.
Mmoja wa wananchi, Adelina Kubalyenda amesena uboreshaji wa bandari utasaidia abiria kupata jengo la kupumzika na kuondoa changamoto waliyonayo sasa abiria akiongeza kuwa hata upanuzi utasaidia kuwepo mzunguko wa fedha.