Sh2.5 trilioni kuifufua reli ya Tazara

Muktasari:

  • Reli hiyo iwapo itaboreshwa inatarajia kuleta ushindani kwa  nyingine itakayounganisha Zambia kwenye bandari ya Lobito hadi Pwani ya Atlantiki ya Angola.

Dar es Salaam. Takriban Dola za Marekani 1 bilioni (zaidi ya Sh2.5 trilioni), zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya matengenezo ya reli ya Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara), yenye umri wa karibu miongo mitano sasa.

Taarifa kuhusu gharama za maboresho ya reli hiyo, imetolewa na Balozi wa China nchini Zambia, Du Xiaohui Februari 8 mwaka huu.

Reli hiyo inayounganisha bandari ya Dar es Salaam kwa upande wa Mashariki na Mji wa Kapiri Mposhi nchini Zambia ni miongoni mwa miradi mikubwa ambayo China ilifadhili ujenzi wake uliokamilika mwaka 1975.

Tangu kukamilika kwa ujenzi wake, miaka 49 iliyopita reli hiyo baadaye ilihitaji matengenezo makubwa ambayo kimsingi ndiyo yatakayofufua ushindani wake.

Katikati ya wiki hii, Xiaohui aliwasilisha pendekezo la mradi wa matengenezo ya reli hiyo kwa Waziri wa Usafirishaji wa Zambia, Frank Tayali.

“Gharama za uwekezaji zitakuja miaka ijayo,” alinukuliwa balozi huyo alipokuwa akizungumza katika matangazo mubashara yaliyorushwa na vyombo vya habari nchini Zambia.

Hata hivyo, hatua ya matengenezo hayo inakuja miezi kadhaa baada ya Serikali ya Tanzania na Zambia kusaini mkataba wa kukabidhi uendeshaji wa reli hiyo kwa kampuni inayomilikiwa na China.

Alipoulizwa na gazeti la The Citizen Februari 9,2024 Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara alimtaka mwandishi wa gazeti hilo kuandaa mahojiano kwa ajili ya ufafanuzi zaidi wa suala hilo.

“Tupange mahojiano kwa ajili ya kulielezea suala hili kwa uzito wake,” alisema Profesa Kahyarara.

Mbali na kauli hiyo ya Kahyarara, The Citizen ilithibitishiwa juu ya kuwasilishwa kwa pendekezo hilo, ingawa bado halijakabidhiwa kwa Serikali ya Tanzania na kwa uongozi wa Tazara.

Uthibitisho huo ulitolewa na Mkuu wa Uhusiano kwa Umma wa Tazara, Conrad Simuchile aliyesema anafahamu kuhusu China kuwasilisha pendekezo, ingawa bado halijafikishwa Tazara.

“Limekabidhiwa wizarani nchini Zambia, lilipaswa kuwasilishwa kwa Tanzania ambaye ni mshirika pia. Tutakuwa na nafasi nzuri ya kuzungumzia hilo baada ya nyaraka hiyo kuwasilishwa kwetu,” alisema.

Desemba 12, mwaka jana, kabla ya China kuwasilisha pendekezo la maboresho ya mradi huo, Tazara ilitangaza kuunda kikosi kazi kutoka kampuni ya uhandisi ya China (CCECC), kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa reli hiyo.

Simuchile alipoulizwa kuhusu kikosi kazi hicho, alijibu tayari kimeshakamilisha kazi yake na taarifa zake ndizo zilizotumika kuandaa pendekezo hilo, linalotarajiwa kuwasilishwa Tazara pia.

Pamoja na jukumu la ukaguzi huo, taarifa ya Tazara ya mwaka jana, ilisema kikosi kazi hicho kilikuwa na jukumu la majadiliano kuhusu masuala muhimu ikiwemo mifumo ya uendeshaji na usimamizi wa mamlaka, mapendekezo ya mpango wa fedha unaosimamiwa na Benki ya Maendeleo ya China (CDB), kodi za ndani, sera na mambo mengine.

Kulingana na taarifa hiyo, kikosi kazi hicho, kilikuwa kikiongozwa na Shirika la Reli ya Ethiopia-Djibout, Peng Danyang, linaloendeshwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Ethiopia na Djibout na CCECC.

"Majadiliano haya yanalenga kuboresha pendekezo la kuifufua Tazara na kuliandaa shirika lizingatiwe na watu wote.

“Mapendekezo hayo yatachunguzwa na Kamati ya Pamoja ya Ufundi ya Tanzania na Zambia, ikifuatiwa na tathmini ya Kamati ya Uongozi ya Tanzania na Zambia na hatimaye, pendekezo lililoboreshwa litawasilishwa kwenye kikosi kazi cha tatu, ambacho kinachojumuisha mawaziri kutoka Serikali ya Tanzania na Zambia, kadhalika mabalozi wa China nchini Tanzania na Zambia,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

China ilijenga na kufadhili ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,860 (maili 1,156) katika miaka ya 1970, lakini tangu ilipoharibika imekuwa ikifanya kazi taratibu.

Reli hiyo iwapo itaboreshwa inatarajia kuleta ushindani na reli nyingine itakayounganisha Zambia kwenye bandari ya Lobito hadi Pwani ya Atlantiki ya Angola.

Zote zikiwa ni sehemu ya juhudi za kupanua njia za usafirishaji nje ya nchi kwa migodi ya shaba na kobalti kutoka Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

China, Tanzania na Zambia zitaifufua reli hiyo kwa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, kulingana na mwakilishi wa Beijing mjini Lusaka.

Tangazo hilo lilikuja siku moja kabla ya Marekani kuwa mwenyeji wa kongamano la uwekezaji katika ukanda wa Lobito nchini Zambia, huku mshauri wa Rais Joe Biden wa masuala ya nishati na uwekezaji, Amos Hochstein na Rais Hakainde Hichilema wakiwa miongoni mwa wazungumzaji wakuu.