Sh474 bilioni hutumika kuagiza mafuta ya kula nje ya Tanzania kila mwaka

Tanzania yaeleza umuhimu wa sekta ya kilimo kukuza uchumi

Muktasari:

Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde amesema kutokana na uzalishaji mdogo wa mafuta ya kula nchini, Serikali imekuwa ikitumia Sh474 kila mwaka kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi kila mwaka.

Mbeya. Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde amesema Serikali ya Tanzania, imekuwa ikitumia Sh474 Bilioni kwa mwaka kwa ajili ya kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi.

Amesema wakati mahitaji ni tani 650,000, uzalishaji wa Tanzania ni kati ya tani 260,000 mpaka 300,000 huku kukiwa na upungufu wa tani 350,000.

Mavunde amesema hayo jana Alhamisi, Agosti 4, 2022 wakati akizungumza kwenye Kongamano la Shamba Darasa lililoandaliwa na Mwananchi Communications Ltd (MCL) kupitia Farm Clinic likilenga kuisukuma ajenda ya 10/30.

Awali, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Daniel Masola alisema ni fedheha kwa taifa kuagiza sukari na mafuta ya kula nje ya nchi wakati kuna uwezekano wa kuzalisha bidhaa hizo ndani ya nchi.

Naibu Waziri Mavunde alisema moja ya kitu kinachowaumiza kwenye hiyo wizara ni kuzalisha mafuta zaidi na kupunguza gharama inayotumika kuagiza nje ya nchi ifikapo mwaka 2030.

Mavunde alisema wameanza kutekeleza mkakati wa kuzalisha mafuta kupitia zao la Alizeti na Mchikichi kwa kualika wawekezaji watakaowekeza kwenye mashamba makubwa.

Kuhusu Kongamano hilo, Mavunde alisema limewafumbua macho na kuwaongezea maarifa ya kutosha.

“Niwaahidi kwa niaba ya wizara ya kilimo, yote yaliyozungumzwa watayachakata na kuyafanyia kazi. Tumepokea ushauri na niwahakikishie kwamba tutakuwa pamoja,” alisema Mavunde.

Akielezea upotevu wa mazao baada ya mavuno, amesema inakadiriwa asilimia 35 yhupotea na kwamba katika kupambana na hilo wameongeza bajeti kwenye ujenzi wa maghar.

“Tumepanga maghala haya kujengwa katika maeneo ya uzalishaji, tunataka wakulima wakizalisha wawe na uwezo wa kuhifadhi mazao yao,” alisema Mavunde.