MCL: Kongamano lijalo tutakwenda shambani kufanya kwa vitendo

Machumu: Mwananchi ni daraja kati ya taasisi za kilimo, mkulima

Muktasari:

Mkurugenzi Mtendaji wawa Kampuni Mwananchi Communications Ltd (MCL), Bakari Machumu amesema wameingia kwenye kilimo kuchochea utoaji wa taarifa sahihi za sekta hiyo na kwamba kongamano lijalo hawatajifungia kwenye kumbi zenye viyoyozi, wataenda shambani

Mbeya. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Bakari Machumu amesema, kampuni hiyo imeingia kwenye kilimo kuchochea utoaji wa taarifa zitakazowasaidia wakulima na wadau kufanya uamuzi sahihi.

Amesema kongamano lijalo litafanyika Mkoani Dodoma na safari hii hawatajifungia kwenye viyoyozi badala yake wataenda shambani kufanya kwa vitendo wakishirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

Juzi, Jumatano Agosti 3, 2022 Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alizindua ushirikiano baina ya MCL, Vodacom na Wizara ya kilimo kupitia Farm Clinic yenye lengo la kusukuma ajenda ya kufikia asilimia 10 ya Kilimo Biashara ifikapo mwaka 2030.

Machumu alisema hayo leo Alhamisi Agosti 4, 2022 wakati akihitimisha Kongamano la Shamba Darasa lililoandaliwa na MCL kupitia Farm Clinic katika ukumbi wa  Tari, Jijini Mbeya ambako yanakofanyika maadhimisho ya Wakulima ya Nanenane.

“Baada ya kongamano hili, tutaandaa makongamano mengine ambayo yatakuwa yanafanyika shambani moja kwa moja tukipita kwenye vituo husika vya Tari,” alisema Machumu.

Machumu alisema kongamano linalofuata litafanyika Dodoma kwenye eneo ambalo Wizara ya Kilimo itatoa maelekezo.

“Kuingia kwetu kwenye kilimo sio kwenda kulima lakini kilimo kinao mnyororo mrefu, tunaingia kwa maana ya kuchochea utoaji wa taarifa sahihi ili watu wapate taarifa na kufanya maamuzi sahihi,” alisema Mchumu.

Kiongozi huyo wa MCL inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, MwanaSpoti na mitandao ya kijamii alisema kampuni hiyo ipo tayari kusaidia katika kusukuma ajenda ya 10/30 kama kauli mbiu ya kampuni hiyo inavyosema.

“Kama kauli mbiu yetu inavyosema, Mwananchi Communications tunawezesha taifa, kilichotokea hapa kinaonyesha ni kiasi gani tunawezesha taifa," alisema na kuongeza:

"Jana, wakati Waziri Bashe akimuelezea Waziri Mkuu, akasema hawa tuna mradi nao wa kuelimisha katika suala la kilimo, akauliza ni hawahawa Mwananchi wa Magazeti? Waziri Bashe akasema ndio, akauliza wameingia kwenye kilimo? Waziri akasema ndio."

Alisema pamoja na Farm Clinic, wameanzisha dawati la kilimo linalotoa machapisho ya kilimo kila Jumamosi kupitia Mbegu ya Dhahabu kwa Mwananchi na Seeds of Gold kwa The Citizen.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde alisema kongamano hilo limewafumbua na kuwaongezea maarifa ya kutosha.

“Niwaahidi kwa niaba ya wizara ya kilimo, yote yaliyozungumzwa watayachakata na kuyafanyia kazi, tumepokea ushauri na tumepokea namna bora ya utekelezaji wa majuku yetu, niwahakikishie ya kwamba tutakuwa pamoja,” alisema Mavunde.