Mataifa 11 kujadili ustawi wa jamii, mapendekezo Dira 2050
Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dk Joyce Nyoni akizungumza kuhusu mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Juni 5 mwaka huu katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere, JNICC. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Jamii, TASAF Shedrack Mziray.
Muktasari:
- Mkutano huo utazalisha mapendekezo ya sera yanayotokana na utafiti, yatakayowasilishwa wizara husika kama mchango wa kitaasisi katika utekelezaji wa awali wa Dira 2050.
Dar es Salaam. Wataalamu, watafiti na watunga sera kutoka nchi 11 wanatarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam kujadili masuala ya ustawi wa jamii, uwezeshaji wa wananchi na maendeleo jumuishi katika kongamano la kwanza la kimataifa la uwezeshaji wa watu na ustawi wa jamii linaloandaliwa na Chuo cha Ustawi wa Jamii.
Kongamano hilo litafanyika Juni 5, 2026 katika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC) na linatarajiwa kuwakutanisha washiriki kutoka Tanzania, Uganda, Nigeria, Namibia, Lesotho, Norway, Hungary, Kenya, Austria, Zimbabwe na Afrika Kusini.
Akizungumza leo Jumatano, Juni 3, 2026 wakati wa kutangaza kongamano hilo, Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dk Joyce Nyoni amesema mkutano huo utakuwa jukwaa la kimataifa la kubadilishana maarifa, tafiti na uzoefu baina ya wasomi, watafiti, watunga sera na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Amesema kongamano hilo lenye kaulimbiu isemayo: “Kuwawezesha Watu na Kubadilisha Jamii: Njia za Kufikia Ustawi Endelevu” litajadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya jamii na ustawi wa wananchi.
“Kongamano hili si tukio la kawaida la kitaaluma. Tunawaleta pamoja wataalamu na watafiti kutoka mataifa mbalimbali ili kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za kuhakikisha maendeleo jumuishi yanayogusa maisha ya wananchi wote,” amesema Dk Nyoni.
Dk Nyoni amesema wataalamu wakuu sita kutoka Norway, Hungary, Namibia, Tanzania, Nigeria na Uganda watawasilisha mada zinazohusu ushiriki wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake, maendeleo na haki za mtoto, ujasiriamali na mabadiliko ya kidijitali, afya ya akili na ustawi wa jamii, elimu ya fedha pamoja na uwezeshaji mahali pa kazi.
Amesema kongamano hilo linafanyika katika kipindi muhimu wakati Tanzania ikijiandaa kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuanzia mwaka wa fedha 2026/27.
“Rais Samia Suluhu Hassan alizindua Dira ya Taifa 2050 mwaka jana. Sasa utekelezaji wake unaanza rasmi Julai 2026. Tuliona ni muhimu kuandaa kongamano hili ili liwe sehemu ya majadiliano ya awali kuhusu namna bora ya kutekeleza maono hayo,” amesema.
Dk Nyoni amesema Dira ya 2050 inaweka msisitizo katika maendeleo ya rasilimali watu, ustawi wa jamii, elimu bora, huduma za afya, ulinzi wa kijamii na fursa za ajira, maeneo ambayo yatajadiliwa kwa kina katika kongamano hilo.
Ameeleza kuwa moja ya matokeo muhimu yanayotarajiwa ni kuzalishwa kwa mapendekezo ya sera yatakayotokana na tafiti na mijadala ya kitaalamu, ambayo yatawasilishwa kwa wizara na taasisi husika kama mchango wa Chuo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.
“Kutokana na kongamano hili tutatoa mapendekezo ya kisera yanayotokana na ushahidi wa kisayansi na tafiti mbalimbali ili kusaidia utekelezaji wa awali wa Dira ya 2050,” amesema.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo anatarajiwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima.