Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shahidi amtaja Diamond kuhusu ahadi ya Sh100 milioni kampeni za Baba Levo

Muktasari:

  • Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando maarufu Baba Levo, anakabiliwa na kesi ya uchaguzi huku Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma ikiendelea kusikiliza ushahidi wa walalamikaji wanaopinga ushindi wake



Kigoma. Shahidi wa 15 katika kesi ya uchaguzi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando maarufu Baba Levo (CCM), amemtaja msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, akidai kuwa aliahidi kutoa Sh100 milioni za kujenga soko wakati wa kampeni za mbunge huyo.

Shahidi huyo Issa Hussein maarufu kama Obama ametoa maelezo hayo katika ushahidi wake wa maandishi uliopokewa mahakamani katika kesi hiyo, leo Ijumaa Julai 10, 2026 wakati akihojiwa maswali ya dodoso na ya kusawazisha.

Katika ushahidi wake huo wa maandishi, shahidi huyo ameeleza kuwa, alikuwa mjumbe wa timu ya kampeni ya mgombea wa ACT- Wazalendo (Zitto Kabwe).

Pia, ndani ya timu hiyo waliunda kamati ndogo ya kufuatilia taarifa na sera za wapinzani wao ili waboreshe mikakati yao na yeye ndiye alikuwa mwenyekiti wa kamati hiyo.

Wakati wa maswali ya dodoso na Wakili wa Serikali Erigh Rumisha, shahidi huyo alipoulizwa kama aliwahi kuwasilisha taarifa hizo katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ameeleza kuwa hakuwasilisha na hafahamu kama vitendo vya rushwa huwa vinachunguzwa na mlalamikaji huwa anachunguzwa.

Hata hivyo, alipoulizwa kama malalamiko yote aliyoyaeleza amewasilisha mahakamani kwa barua kuthibitisha kuwa aliyawasilisha kwa msimamizi wa uchaguzi, amejibu kuwa aliandika na kwenye maelezo yake amezinukuu.

Katika ushahidi wake huo ameeleza kuwa, katika mkutano wa kufunga kampeni Kata ya Kimpapa alikuwepo Baba Levo na wasanii wengi akiwamo Diamond Platnumz, ambaye aliahidi kutoa Sh100 milioni za kujenga soko.

Katika mahojiano yake na wakili wa Baba Levo, Thomas Msasa, alipoulizwa kama kutoa ahadi ni rushwa, shahidi huyo amejibu kuwa si tu rushwa, bali ni rushwa ya wazi.

Hata hivyo, alipoulizwa kama kweli mgombea wa ACT-Wazalendo aliahidi kutoa Sh1 bilioni kwa kina mama, amekiri kuwa ni kweli lakini akafafanua kuwa Zitto aliahidi kutoa kama atachaguliwa.

Katika ushahidi wake wa maandishi, ameeleza taarifa za rushwa na matendo yasiyo ya maadili katika mkutano uliofanyika Septemba 25, 2025 Kibirizi.

Awali, Baba Levo alitangazwa mbunge wa Kigoma Mjini katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akimshinda mpinzani wake kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Zitto Kabwe.

Hata hivyo, wananchi wanne wanaojitambulisha kama wapigakura wa Kigoma Mjini, Johary Kabourou, Luma Akilimali, Pendo  Kombolela,  Lumu  Mwitu  wamefungua kesi kupinga ushindi huo.

Walalamikiwa wengine katika kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025 ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Walalamikaji wanadai uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki, kwa kuwa uligubikwa na kasoro nyingi za ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, vikiwamo vitendo vya rushwa na udini vilivyofanywa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.

Hivyo, wanaiomba Mahakama hiyo iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.

Wakati akiongozwa na wakili wa walalamikaji, John Seka amefafanua kuwa katika kipindi cha kampeni kuna mambo yanayokatazwa na yakifanyika huhesabika kama rushwa na kwamba kitendo cha Diamond kuahidi kutoa Sh100 milioni ni rushwa.

Awali, shahidi wa 14 katika kesi hiyo, Majid Ushamu  ameieleza Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma kuwa siku ya uchaguzi alitekwa na watu asiowajua akiwa katika kituo cha kupigia kura saa sita usiku.

Ametoa maelezo katika ushahidi wake wa maandishi uliopokewa mahakamani kuwa sehemu ya ushahidi wake katika kesi hiyo leo Ijumaa Julai 10, 2026 wakati akihojiwa maswali ya dodoso.

Shahidi huyo ameeleza kuwa,  alikuwa wakala wa majumuisho na kwamba wakati wa kuhesabu kura alibaini kuwa karatasi nyingi za kura zilionekana kupigwa na mtu mmoja.

Lakini, wakati akihojiwa maswali ya dodoso na Wakili wa Serikali Mwandamizi George Kalenda, kama ana utaalamu wa kuthibitisha kura halali na haramu, amejibu kuwa si mtaalamu, lakini alibaini hali hiyo kutokana na alichokiona.

Amedai katika maelezo yake kuwa, akiwa kituoni ghafla lilifika gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye rangi nyeupe wakashuka watu wakamteka na kumwingiza ndani ya gari na kuondoka naye.

Hata hivyo, akihojiwa na wakili Kalenda amejibu kuwa hakutaja namba ya gari hilo na kwamba hakuwataja watu hao waliomteka kwa kuwa, hakuwa anawafahamu, lakini hawakuwa wamevaa sare za polisi wala hawakusema kuwa wana uhusiano na polisi wala Baba Levo, wala msimamizi wa uchaguzi.

Alipoulizwa kama alikwenda kutoa taarifa za kutekwa kwake polisi, amejibu kuwa hakwenda kutoa taarifa polisi.

Katika maelezo yake ameeleza kuwa alitoa taarifa hizo kwa aliyekuwa meneja wa kampeni wa mgombea wa ACT-Wazalendo  Abdul Nondo, lakini alipoulizwa kama Nondo  ana vyombo vya uchunguzi wa matukio ya utekaji au kama anamiliki jeshi, amejibu kuwa hana.

Pia, alipoulizwa kama amewasilisha mahakamani kura alizodai kuwa si halali amejibu kuwa hajaziwasilisha.

Wakati akihojiwa na wakili Msasa wa Baba Levo, kuhusu kutekwa kwake kama katika maelezo yake ya maandishi ameleza alitekwa tarehe ngapi na muda gani, amejibu hakuna tarehe aliyoitaja.

Katika ushahidi wake wa maandishi amedai kuwa kwa mujibu wa wakala wa ACT-Wazalendo katika kituo chake, kura hazikuhesabiwa.

Hata hivyo, akiongozwa na wakili wa walalamikaji, John Seka kutoa ufafanuzi wa majibu yake kwa maswali ya dodoso, shahidi huyo  ameeleza kuwa hakuweza kuleta mahakamani kura haramu kwa kuwa, yeye hakuwa msimamizi wa uchaguzi wala mwakilishi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ((INEC)).

Kuhusu kutoa taarifa za kutekwa kwake kwa Nondo badala ya polisi, ameeleza kuwa Nondo si mamlaka bali alipeleka kwake taarifa kwa kuwa ni kiongozi na kwamba angeweza kushauri cha kufanya.

Kuhusu kutokutaja namba za gari lililomteka ameeleza kuwa, hakuweza kuona namba kwa kuwa alikuwa hajajiandaa akifafanua kuwa gari hilo lilifika tu kituoni hapo wakashuka watu wakamkamata na kumwingiza ndani ya gari.