Prime
Shahidi kesi ya Baba Levo aeleza alivyofukuzwa kituoni, kuwekwa mahabusu
Muktasari:
- Mbunge wa Kigoma Mjini, maarufu Baba Levo, anakabiliwa na kesi ya uchaguzi ambayo imeendelea kusikilizwa ushahidi wa upande wa walalamikaji wanaopinga ushindi wake.
Kigoma. Shahidi wa 13 katika kesi ya uchaguzi inayomkabili mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando, maarufu Baba Levo (CCM), ameieleza Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Kigoma, jinsi alivyofukuzwa kituoni na kuwekwa mahabusu siku ya uchaguzi.
Shahidi huyo, Kassim Omary, mkazi wa Ujiji, Manispaa ya Kigoma Mjini, ametoa maelezo hayo katika ushahidi wake wa maandishi uliopokewa mahakamani na kuwa sehemu ya ushahidi wake katika kesi hiyo leo, Ijumaa Julai 10, 2026.
Baba Levo alitangazwa mbunge wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akimshinda mpinzani wake mkubwa kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Zitto Kabwe.
Hata hivyo, wananchi wanne wanaojitambulisha kama wapigakura wa Jimbo la Kigoma Mjini, Johary Kabourou, Luma Akilimali, Pendo Kombolela na Lumu Mwitu, wanapinga ushindi wake.
Kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025, mbali na Baba Levo ambaye ni mlalamikiwa wa pili katika kesi hiyo, walalamikiwa wengine ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Walalamikaji hao wanadai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwa kuwa uligubikwa na kasoro nyingi za ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, vikiwemo vitendo vya rushwa na udini vilivyofanywa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.
Hivyo, wanaiomba Mahakama hiyo, pamoja na mambo mengine, iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.
Katika ushahidi wake huo wa maandishi, shahidi huyo ameeleza kuwa alikuwa wakala wa ACT-Wazalendo, lakini siku ya uchaguzi alikamatwa na polisi na kupelekwa mahabusu, hivyo kituo kubakia bila wakala wa mgombea wao.
Hata hivyo, wakati wa maswali ya dodoso, alipoulizwa na Wakili wa Serikali, George Kalenda, ameeleza kuwa hajawasilisha mahakamani barua ya uthibitisho kuwa alikuwa wakala.
Alipoulizwa kama amekuja kutoa ushahidi katika kesi ya uchaguzi au kuhusu kukamatwa kwake na kupelekwa mahabusu, amejibu kuwa amekuja kutoa ushahidi wa kesi ya uchaguzi na wa kukamatwa kwake na kupelekwa mahabusu.
Katika maelezo yake ameeleza kuwa alitolewa nje ya kituo baada ya kukutwa na Daftari la Wapigakura.
Hata hivyo, amekiri kuwa katika maelezo hayo hakuna mahali alipoandika kuwa aliomba na akanyimwa fomu ya malalamiko iitwayo Fomu ya Kuridhika na Kutokuridhika kwa Wakala Kabla na Baada ya Uchaguzi (Fomu Na. 14).
Vilevile, ameeleza kuwa mawakala wengine aliokuwa nao katika kituo cha kupigia kura walitoa malalamiko yao tofauti, lakini amekiri kuwa hajawataja kwa majina mawakala hao waliotoa malalamiko hayo.
Kuhusu madai ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu, amekiri kuwa, japokuwa hakuwasilisha mahakamani rejesta ya polisi kuthibitisha kuwa aliwekwa mahabusu.
Pia, ameeleza kuwa, japokuwa alikuwa na maumivu, hakwenda hospitalini.
Vilevile, ameeleza kuwa kuna kura ziliingizwa katika masanduku ya kura na wasimamizi wa uchaguzi.
Wakati akihojiwa na wakili wa Baba Levo, Thomas Msasa, kuhusiana na madai yake kuwa wasimamizi wa uchaguzi waliingiza kura, kama ni habari za kuambiwa kwa kuwa tayari wakati huo hakuwepo kituoni baada ya kukamatwa na kupelekwa polisi, amejibu kuwa si habari za kuambiwa.
Wakati akihojiwa na wakili wa walalamikaji, John Seka, katika kutoa ufafanuzi wa majibu yake kwenye maswali ya dodoso, ameeleza kuwa hakuwasilisha mahakamani rejesta ya polisi kuthibitisha kukamatwa kwake kwa kuwa yeye si polisi.
Pia, amefafanua kutokuwasilisha fomu ya malalamiko kwa kueleza kuwa wakati fomu hizo zilipotolewa hakuwepo kituoni kwa kuwa tayari alikuwa kituo cha polisi.